ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 26, 2020

Tshishimbi, Deo Kanda mtegoni

By MAJUTO OMARY, Mwanaspoti
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limewaweka mtegoni nyota wa kigeni wanaocheza nchini kwani wamepanga kuweka kanuni zitakazowabana wale wasiozichezea timu zao za taifa, kuweza kusajiliwa nchini kuanza mwezi ujao.

Kwa sasa Tanzania ina nyota wa kigeni karibu 70, lakini wengi wao hawazichezei timu zao za taifa wakiwamo, kina David Molinda, Papy Tshishimbi, Gnamien Gislain Yikpe wa Yanga ama Pascal Wawa, Deo Kanda na Wabrazili Gerson Fraga na Tairone de Santos wanaokipiga Simba.
Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Oscar Mirambo amesema mapema leo Jumapili kuwa, hatua hiyo ni kuendelea kuiboresha Ligi Kuu yaTanzania Bara na hasa baada ya taarifa ya Waziri wa Michezo, Harrison Mwakyembe aliyeiagiza Baraza la Michezo kujadili na wadau soka kuhusiana na wingi wa wachezaji wa kigeni.

Mirambo amesema mara kadhaa wamekuwa wakisisitiza Ligi Kuu Bara si kichaka cha kujificha kwa wachezaji wa kigeni ambao baadhi yao hawana tija katika maendeleo ya mpira wa miguu.
Amesema kuna baadhi ya wachezaji wa kigeni hawana uwezo kabisa kulinganisha na wachezaji wa nyumbani pamoja na kusajiliwa kwa fedha nyingi.

Amefafanua katika vikao vya kujadili kanuni za msimu husika, wamekuwa wakisisitiza wachezaji wenye uwezo mkubwa na wanachezea timu zao za taifa ndiyo wapewe kipaumbele cha kusajiliwa na vilabu vimekuwa vikifanya tofauti.

Mirambo amesema soka ni mchezo wa wazi kwa kuonekana viwango vya wachezaji na kufikia wakati unahoji vigezo vilivyotumika kumsajili mchezaji ambaye anaonyesha kiwango cha chini kabisa kulinganisha na wazawa.

“Ili kuboresha ligi yetu, tutaweka kipengele hicho katika kanuni zetu na kukifanyia kazi wakati wa usajili. Naamini klabu zitaelewa wanamaanisha nini,” amesema Mirambo.
Amesema TFF haipangi kanuni za Ligi Kuu peke yake na kabla ya kuanza kwa msimu, ukutana na klabu zote kujadili kanuni za ligi, changamoto na mambo mengine.

“Timu uombwa kutoa mapendekezo yake kuhusiana na kanuni za ligi kuu na ufanya hivyo kwa maandishi na baadaye kujadiliwa katika kikao cha pamoja,” amesema.

Amesema hata idadi ya wachezaji wa kigeni kuwa 10 ilipitishwa kwa pamoja na klabu pamoja na ukweli kuwa mpaka sasa hakuna klabu hata moja iliyosajili wachezaji 10.

Timu tatu mpaka sasa zimekaribia kufikisha idadi ya wachezaji hao 10 ambazo ni Azam FC na Yanga zenye wachezaji tisa kila mmoja na Simba yenye wachezaji nane.

Yanga ina Farouk Shikhalo (Kenya), Lamine Moro (Ghana), Papy Tshishimbi (DR Congo), Erick Kabamba (Zambia), Bernard Morrison (Ghana), David Molinga (DR Congo), Yikpe (Ivory Coast), Haruna Niyonzima na Patrick Sibomana (Rwanda).

Simba yenyewe ina Wawa (Ivory Coast), Clatous Chama (Zambia), Deo Kanda (DR Congo), Francis Kahata (Kenya), Meddie Kagere (Rwanda), Luis Miquissone (Msumbiji), Fraga na Tairone (Brazili).
Upande wa Azam ikiwa na Razack Abarola (Ghana), Nicholas Wadada (Uganda), Bruce Kangwa (Zimbabwe), Daniel Amoah (Ghana), Donald Ngoma na Never Tegere (Zimbabwe), Obrey Chirwa (Zambia), Richard Djodi (Ivory Coast) na Yakubu Mohammed (Ghana), huku ikimtoa kwa mkopo Emmanuel Mvuyekure kwa klabu ya KMC.

Klabu nyingine zenye nyota wa kigeni ni Namungo, Singida United, KMC, Biashara United na Mwadui FC.

No comments: