Thursday, April 16, 2020

Uchaguzi mkuu ni mtifuano Chadema

By Ibrahim Yamola, Mwananchi

Ni mtifuano. Ndivyo unavyoweza kuelezea kile kitakachojiri ndani ya Chadema utakapowadia wasaa wa kutafuta wagombea ubunge wa chama hicho katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Hali hiyo inatokana na kuhitimishwa kwa utiaji nia wa wanachama wa chama hicho katika majimbo huku baadhi ya wabunge wa majimbo na viti maalum wakitarajiwa kuonyeshana umwamba wa nani zaidi ya mwenzake.

Hadi muda uliokuwa umetolewa na Katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika kwa wale wanaotaka kugombea kuandika barua kwake kupitia ofisi za kanda ulipotimia Machi 30, wabunge wake wanne hawajajitokeza kutia nia jimbo lolote.

Januari 29, Mnyika alitangaza kufungua pazia la uchaguzi mkuu akiwataka wanachama wanaotaka kuwania ubunge kuandika barua ofisi ya katibu mkuu kupitia kanda za chama hizo huku udiwani kupitia wilaya na urais kuandikwa kwake.

Wabunge hao ni; Joseph Selasini (Rombo), Wilfred Lwakatare (Bukoba Mjini) na Jaffar Michael (Moshi Mjini) ambaye alikwisha kutangaza kutogombea tena na Anthony Komu (Moshi Vijijini) hivi karibuni aliweka wazi kuwa mara baada ya Bunge kumalizika atatimkia NCCR-Mageuzi.

Mwananchi lilipomtafuta Selasini alisema, “mimi bado natafakari huku Rwakatare akisema “mwaka huu sigombei napumzika” na mwaka mmoja na nusu uliopita aliwaeleza wananchi wa jimbo lake kuhusu adhma hiyo.

“Nilianza harakati za kisiasa mwaka 1992 hadi sasa na mara zote niligombea. Ni wakati wa kuwaachia wengine wakaendeleza tulipoachia,” alisema Rwakatare.

Mwananchi linaichambua orodha na baadhi ya majina ya waliotia nia kwenye kanda kumi za Chadema wamo watumishi wa umma ambao, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema anasema, “kwa sasa hatutaweka wazi majina yao hadi muda utakapofika.”

Mrema alisema kwamba hadi Machi 30, mwitikio umekuwa mkubwa kwa udiwani na ubunge hali inayoonyesha ukomavu wa chama na hakuna aliyejitokeza kutia nia ya kuwania urais.

Alisema mchakato wa kura za maoni utatangazwa hapo baadaye.

Chadema wakiwa hatua hiyo, baadhi ya vyama vingine kama CCC, ACT- Wazalendo, CUF, NCCR- Mageuzi, CCK na Chaumma bado havijaanza michakato ya kupata wagombea.

Vigogo kuumana Dar es Salaam

Kanda ya Pwani yenye majimbo 19 yanayohusisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani wagombea waliojitokeza ni 72.

Jimbo la Ubungo waliojitokeza ni saba kati yao ni mbunge wa sasa, Saed Kubenea na Meya wa Ubungo, Boniface Jacob ambaye tayari ametangaza kutogombea udiwani alioutumikia kwa miaka kumi mfululizo.

Ukonga wako saba akiwamo Asia Msangi aliyegombea uchaguzi mdogo na Mwita Waitara wa CCM lakini akashindwa. Pia, yupo Omary Sweya ambaye ni mwenyekiti wa Chadema jimbo hilo.

Mbagala wamejitokeza wanne, Temeke (6), Kigamboni wawili akiwamo mbunge wa viti maalum, Lucy Mageleli; Kinondoni wanne wakiwamo mbunge wa viti maalum, Susan Lyimo na Mustapha Muro ambaye ni diwani wa Kinondoni.

Ilala wamejitokeza wanane akiwamo Gervas Lyenda ambaye ni ofisa habari wa kanda ya Pwani. Halima Mdee atachuana na wengine wawili jimbo la Kawe akiwamo Joel Mwakalebela.

Mnyika yeye atakuwa na kibarua cha kuwakabili wenzake wawili huko Kibamba ambao ni madiwani.

Shughuli nyingine itakuwa Segerea ambako wamejitokeza 10, kati yao ni madiwani na kata zao kwenye mabano, Patrick Asenga (Tabata), Manase Mjema (Kimanga) na John Mrema ambaye ni mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema.

Jimbo la Kibaha Mjini wamejitokeza wanne, Kisarawe wawili, Mafia mmoja, Chalinze wawili, Kibiti mmoja, Bagamoyo wawili, Rufiji mmoja, Kibaha vijijini wawili na Mkuranga wawili akiwamo Baraka Mwango ambaye ni kaimu mwenyekiti wa Kanda ya Pwani wa chama hicho.

Kanda ya Nyasa kutashuhudia mtifuano wa wabunge wawili wa chama hicho, David Silinde aliyetia nia jimbo la Tunduma linaloongozwa sasa na Frank Mwakajoka.

Silinde alikuwa Momba ambako waliojitokeza kugombea ni wawili.

Vwawa wamejitokeza wanne akiwamo Fanuel Mkisi. Kwa sasa jimbo hilo linaongozwa na waziri wa kilimo, Japhet Hasunga. Ileje wamejitokeza wawili sawa na Songwe.

Mbozi wamejitosa wanne akiwamo mbunge wa sasa wa chama hicho, Paschal Haonga.

Mkoani Rukwa katika jimbo la Sumbawanga Mjini wako (4), Nkasi Kusini na Kaskazini kote wamejitosa wawili, Kyerwa wamejitokeza wanne akiwamo Daniel Naftal aliyegombea tena jimbo hilo mwaka 2015.

Kalambo wako wawili

Katika Mkoa wa Njombe, jimbo la Njombe Mjini wamejitokeza watano akiwamo katibu wa kanda hiyo ya Nyasa, Emmanuel Masonga, Makambako, Lupembe, Ludewa na Wang’ing’ombe kote wamejitosa wawili wawili huku Makete akiwa mmoja ambaye ni Jackson Mbogela.

Msigwa, Sugu wakosa wapinzani

Mchungaji Peter Msigwa amekosa mpinzani Iringa Mjini; Mufindi Kusini na Kaskazini wakijitokeza wawili wawili huku Kilolo wakijitosa watano jimbo linaloongozwa na Vanance Mwamoto wa CCM.

Mafinga Mjini amejitokeza mmoja, William Mungai ambaye ni mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Iringa na mtoto wa marehemu Joseph Mngai aliyewahi kuwa waziri wa elimu.

Isimani, jimbo linaloongozwa na waziri wa ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi, William Lukuvi amejitokeza mmoja, Patric Ole Sosopi aliyekuwa mwenyekiti wa vijana wa Chadena (Bavicha) huku Kalenga nako akijitokeza mmoja Grace Tendega ambaye ni Katibu wa Baraza la Wanawake wa chama hicho (Bawacha).

Jimbo la Mbeya Mjini amejitokeza mmoja ambaye ni mbunge wa sasa, Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu huku mchuano ukitarajiwa kushuhudiwa Rungwe ambako wamejitokeza watano wakiwamo mbunge wa viti maalum, Sophia Mwakagenda na Ahombokela Mwatenda.

Mbeya Vijijini, Lupa na Mbarali, majimbo yanayoongozwa kwa sasa na CCM wamejitokeza wawiliwawili huku Busokelo wakiwa watatu na Kyela kwa waziri wa habari, utamaduni, sanaa na michezo, Dk Harrison Mwakyembe wakijitoza watano.

Kanda ya Serengeti yenye mikoa mitatu ya Simiyu, Mara na Shinyanga nako kutakuwa na mchuano mathalani Tarime Vijijini, John Heche atakuwa na kibarua cha kuchuana na Moses Misiwa ambaye ni mwenyekiti wa halmashauri ya Tarime Vijijini. Bunda Mjini amejitokeza mmoja ambaye ni mbunge wa sasa, Ester Bulaya sanjari na Tarime Mjini, Esther Matiko anayeendelea kuongoza jimbo hilo akiwa pia ndiye mwenyekiti wa kanda ya Serengeti. Rorya na Mwibara wamejitokeza wawiliwawili, Butiama watatu na Bunda Vijijini mmoja. Serengeti wamejitokeza wanne akiwamo mbunge wa viti maalum, Catherine Ruge.

Musoma Mjini wamejitoza watano wakiwamo Julius Mwita aliyekuwa katibu mkuu wa Bavicha na Joyce Sokombi ambaye ni mbunge wa viti maalumu.

Maswa Mashariki, Maswa Magharibi, Kisesa, Busega kwa Dk Raphael Chegeni wa CCM kote wamejitoza wawiliwawili.

Itilima wamejitokeza watatu akiwamo mbunge wa viti maalum, Gimbi Masaba, Bariadi kunakoongozwa na Andrew Chenge wa CCM wamejitosa watatu sawa na Meatu.

Shinyanga kwenye majimbo matano kutashuhudia patashika katika jimbo la Shinyanga Mjini linaloongozwa na Stephen Masele wa CCM, wamejitokeza tisa akiwamo mbunge wa viti maalum, Salome Makamba.

Kahama Mjini, Ushetu na Solwa wamejitosa wawiliwawili kila sehemu huku Kishapu wakijitokeza watatu.

Visiwani Zanzibar katika Kanda ya Ungunja hakuonyeshi kama kutakuwa na mchuano mkali hasa ikizingatiwa katika majimbo ya Kijitoupele, Mtoni, Mfenesini, Mpendae na Kikwajuni akijitokeza mmojammoja huku Mpendae, Amani na Chumbuni wakijitosa wawiliwawili. Kanda ya Kaskazini yenye mikoa ya Manyara, Tanga, Kilimanjaro na Arusha inaonyesha Freeman Mbowe wa Hai na Godbless Lema wa Arusha Mjini wakiwa hawana wapinzani. Rombo wamejitokeza wawili, Vunjo kwa James Mbatia wa NCCR-Mageuzi wamejitosa watatu akiwamo mbunge wa viti maalum, Grace Kiwelu; Moshi Mjini amejitokeza mmoja ambaye ni Kollins Tamimu sawa na Moshi Vijijini aliyejitosa mbunge wa viti maalum, Lucy Owenya. Same Magharibi wamejitokeza wawili, Same Mashariki nako wawili akiwamo mbunge wa sasa, Naghenjwa Kaboyoka ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC). Siha wamejitokeza wawili.

Arumeru Mashariki wamejitokeza watatu wawili waliwahi kuwa wabunge ambao ni Joshua Nassary aliyekuwa akiongoza jimbo hilo na Rebecca Mdogo wa viti maalum.

Monduli amejitokeza mmoja ambaye ni Moses Laizer sawa na Longido na Ngorongoro. Karatu wamejitokeza watano wakiwamo wabunge ambao ni Cecilia Pareso na mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Willy Qambalo na mwanasheria Samuel Welwel huku Simanjiro akijitokeza mmoja Emmanuel Landeyi.

Majimbo ya Hanang’, Mbulu mjini na Mbulu Vijijini kote wamejitokeza wawiliwawili. Babati Mjini kunakoongozwa na Pauline Gekul aliyekuwa mbunge wa Chadema kabla ya kutimkia CCM na kuchaguliwa tena wamejitokeza wawili akiwamo mbunge wa viti maalum, Anna Gidarya.

Tanga hali si shwari kwa Chadema kwani majimbo ya Pangani, Mkinga, Handeni Mjini, Mlalo na Handeni Vijijini hakuna aliyejitokeza kutia nia huku Tanga Mjini, Lushoto, Korogwe Mjini, Korogwe Vijijini kila sehemu amejitokeza mmojammoja. Muheza pekee ndiko wamejitokeza watatu akiwamo mbunge wa viti maalumu, Yoseph Komba.

Kanda ya Kusini yenye mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi nako kutashuhudia mchuano wa hapa na pale kwa baadhi ya majimbo ambapo Lindi Mjini, aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo kupitia CUF, Salum Barwany atachuana na Hemed Ali ambaye ni katibu wa Chadema Kanda ya Pwani.

Barwany ambaye sasa ni makamu mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini alikuwa mbunge kati ya mwaka 2010-15.

Mtama kunakoongozwa na Nape Nnauye wa CCM amejitokeza mmoja Seleman Mathew ambaye ni mwenyekiti wa kanda hiyo na aliyegombea uchaguzi mkuu uliopita. Kilwa Kusini kwa Seleman Bungara maarufu ‘Bwege’ wa CUF amejitokeza mmoja sanjari na majimbo ya Nachingwea, Tandahimba, Nanyamba, Lulindi, Newala Vijijini, Ndanda, Newala Mjini, Nyasa na Mchinga kunakoongozwa na Hamidu Bobali wa CUF.

Mtwara Mjini wamejitosa watatu akiwamo mbunge wa viti maalum, Tunza Malapo huku Mbinga Mjini, Mbiga Vijijini, Namtumbo wamejitokeza wawiliwawili kila sehemu. Peramiho kwa Waziri wa nchi, ofisi ya waziri mkuu, sera, bunge, kazi, ajira na wenye ulemavu, Jenista Mhagama wakijitosa watatu.

Songea wamejitokeza sita wakiwamo Mchungaji Stella Mapunda na Sanetor Yatembo; Tunduma Kaskazini kajitosa mmoja ambaye ni mbunge wa viti maalum, Zubeda Sakuru, Liwawe nako amejitokeza mmoja, mbunge wa viti maalum, Ratifa Chande.

Masasi Mjini wamejitokeza wawili huku jimbo la Ruangwa linaloongozwa na waziri mkuu, Kassim Majaliwa amejitokeza mmoja Halima Lichongo sawa na Nanyumbu alikojitokeza mmoja pekee.

Kanda ya Magharibi inayojumuisha mikoa ya Katavi, Kigoma na Tabora kumeshuhudia aliyekuwa mbunge wa Muhambwe kupitia NCCR-Mageuzi kuanzia 2010-2015, Felix Mkosamali akijitosa kwenye jimbo hilo tena kupitia Chadema.

Mkosamali ambaye uchaguzi wa 2015 alishindwa akiwa NCCR-Mageuzi na Atashasta Nditiye wa CCM, atachuana na wengine watatu akiwamo, Arcado Ntagazwa ambaye ni mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini na mjumbe wa kamati kuu. Kasulu Vijijini amejitokeza Yona Nzegera, Kigoma Mjini amejitosa mbunge wa viti maalumu, Sabreena Sungura, Kigoma Kaskazini na Kasulu Mjini nako kuna mmojammoja sawa na Kigoma Kusini. Buyungu kwa Christopher Chiza wa CCM wamejitosa watatu huku Manyovu wakiwa wawili. Mpanda Mjini amejitokeza mmoja mbunge wa viti maalum, Rhoda Kunchela, Kavuu linaloongozwa na Dk Pudenciana Kikwembe wa CCM amejitokeza mmoja huku Mpanda Vijijini na Nsimbo wakijitosa wawiliwawili. Bukene amejitokeza mmoja, Lumola Kahumbi ambaye ni mdogo wake na waziri wa maliasili na utalii, Dk Hamisi Kigwangalla. Zenga Vijijini, Igalula, Manonga kote wamejitokeza wawiliwawili huku Tabora Mjini akijitosa mmoja ambaye ni mbunge wa viti maalum, Hawa Mwaifunga.

Kaliua na Sikonge wamejitosa mmojammoja huku Nzega Mjini linaloongozwa na naibu waziri wa kilimo, Hussen Bashe wamejitokeza wawili akiwamo Ally Nnyuze.

Kanda ya Victoria kuna mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera kutashuhudia mtifuano wa kutosha tu ikiwamo Nyamagana ambapo Ezekiel Wenje aliyekuwa mbunge 2010-2015 kisha kushindwa mwaka 2015 amekuwa miongoni mwa wanne walioitia nia.

Ilemela wamejitokeza saba wakiwamo, mbunge wa viti maalum, Susan Masele, Jackson Manyerere aliyekuwa meya 2010-2015 na Gasper Manalyela huku Sumve wakiwa watatu, Buchosa mmoja, Kwimba na Misungwi wawiliwawili.

Magu wako sita akiwamo Kalwinzi Ngongoseke, Ukerewe saba akiwamo Salvatory Machemri aliyekuwa mbunge 2010-2015 na mwaka 2015 alitimkia ACT-Wazalendo lakini akashindwa na sasa yuko Chadema.

Bukoba Mjini wamejitokeza wawili akiwamo Cheif Karumuna ambaye ni Meya wa Bukoba Mjini. Muleba Kaskazini nako kuna wawili akiwamo Dastan Mutogaywa. Muleba Kusini alikokuwa anaongoza Profesa Anna Tibaijuka ambaye amekwisha kutangaza kutogombea wamejitokeza wawili Rodrick Lutembeka ambaye ni katibu mkuu wa baraza la wazee wa Chadema na Merchadi Lizire ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Kagera.

Biharamulo kuna watatu, Karagwe wawili sawa na Kyerwa akiwamo mbunge wa viti maalum Anatropia Theonest. Geita Mjini wamejitoza wawili, Busanda nako wawili akiwamo mbunge wa viti maalum, Upendo Peneza, Bukombe wawili akiwamo Renatus Nzemo huku Geita Vijijini na Nyang’hwale mmoja sawia na Chato kunakoongozwa na Dk Medard Kalemani wa CCM ambaye ni Zacharia Obaidi.

Kanda ya Kati inayojumuisha mikoa Morogoro, Singida na Dodoma imeacha maswali jimbo la Singida Mashariki lililokuwa likiongozwa na Tundu Lissu ambalo hakuna aliyejitosa kutia nia. Singida Magharibi, Manyoni Magharibi wako wawili sawa na Singida Mjini.

Lissu ambaye ni makamu mwenyekiti wa Chadema- Bara aliyeko Ubelgiji alipoulizwa kulikoni hajatia nia alisema “muda bado, ukifika utaamua.”

Singida Kaskazini wamejitosa wawili akiwamo David Djumbe huku Iramba Magharibi linaloongozwa na Dk Mwigulu Nchemba wa CCM amejitokeza mmoja mbunge wa viti maalum, Jesca Kishoa.

Morogoro Mjini wako watano akiwamo mbunge wa viti maalum, Devotha Minja, Ulanga watatu, Morogoro Kusini mmoja ambaye ni Pesa M Pesa, Mikumi mmoja mbunge wa sasa, Joseph Haule maarufu ‘Profesa J’, Mlimba mmoja mbunge wa sasa, Susan Kiwanga sawa na Kilombero mbunge wa sasa Peter Lijualikali.

Mvomero wawili, Morogoro Kusini Mashariki mmoja, Kilosa wawili na Gairo mmoja ambaye ni Kashikashi Rugowoka. Dodoma Mjini wamejitokeza watatu akiwamo Benson Kigaila ambaye ni naibu katibu mkuu - Bara.

Mpwapwa wamejitokeza wawili sawa na Kongwa kunakoongozwa na Spika Job Ndugai ambao ni Edson Mbena na Neema Chinyo. Kondoa Mjini wawili, sawa na Mtera kwa Livingstone Lusinde wa CCM ambaye ni Amina Hassan. Chemba amejitokeza mmoja.

No comments: