Friday, April 17, 2020

Wagonjwa wa Corona Tanzania Wafikia 147

IDADI ya kesi za wagonjwa wa Covid 19 nchini Tanzania imeongezeka na kufikia kesi 147, baada ya wagonjwa wengine wapya 53 kukutwa na virusi vya Corona.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema wagonjwa hao wote ni Watanzania ambapo 38 ni kutoka mkoa wa Dar es Salaam, Zanzibar wagonjwa 10, Kilimanjaro mgonjwa mmoja, Mwanza mgonjwa mmoja, Pwani mgonjwa mmoja, Lindi mgonjwa mmoja na Kagera mgonjwa mmoja.

“Mnaweza kuona nimetoa takwimu kubwa sana lakini tumeamua tuseme ukweli kwa sababu watanzania sasa lazima waelewe kuwa tunakabiliwa na changamoto kubwa.

Waziri wa afya Tanzania Ummy Mwalimu amewataka watanzania kuchukua tahadhari kubwa kujilinda dhidi ya ugonjwa wa Corona. “Kama kuna mmoja alikuwa na shauku basi ni wakati afahamu Corona inaanza na wewe kujikinga na pia uwakinge wengine.”

Aidha, Ummy mwalimu amesema jumla ya wagonjwa waliopona mpaka sasa ni 11 huku wagonjwa watano wakipoteza maisha tangu ugonjwa huop uingie hapa nchini.

No comments: