ANGALIA LIVE NEWS

Friday, February 5, 2021

WAZIRI MKUU ATOA SIKU TATU RIPOTI YA WATUMISHI WANAOISHI NJE YA VITUO VYAO IMFIKIE

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akijibu maswali katika kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma, Februari 4, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameipa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ifuatilie Halmashauri zilizopaswa kuhamia kwenye maeneo yake na impatie taarifa ifikapo Jumamosi, Februari 6, 2021.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Februari 4, 2021) wakati akijibu swali la mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu bungeni jijini Dodoma.

Mbunge huyo alitaka kujua Serikali inatoa kauli gani kuhusu watumishi hao walioshindwa kutii agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli alilolitoa Oktoba 24, 2019 akiwataka wahamie kwenye makao makuu ya Halmashauri zao kabla ya Oktoba 30, 2019.

Bw. Musukuma amesema kitendo hicho kinaitia Serikali hasara kwani watumishi hao walihamisha ofisi tu kwenda makao makuu ya Halmashauri lakini wanaendelea kuishi mijini.

Waziri Mkuu amesema anahitaji kupata taarifa juu ya halmashauri ambazo watumishi wake wanaishi nje ya vituo vyao vya kazi ili hatua za kinidhamu zichukuliwe. “Serikali inataka watumishi wote waishi kwenye vituo vyao vya kazi ili waweze kuwahudumia wananchi kwa ukaribu.”

Amesema anatambua uhaba wa nyumba za watumishi uliopo lakini kwenye makao makuu ya Halmashauri kuna nyumba za wenyeji ambazo watumishi hao wanaweza kupanga ili waweze kutoa huduma karibu na wananchi wanaowaongoza.

Kufuatia hatua hiyo, Waziri Mkuu amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa wasimamie na kuhakikisha watumishi wote wanaoishi nje ya vituo vyao vya kazi wanaondoka mara moja na kuhamia katika maeneo husika. “Simamieni watumishi hao waondoke mara moja, baada ya tamko hili. Hatuwezi kuwapa muda zaidi sababu umeshapita. Endapo hawatafanya hivyo, Mkuu wa Mkoa husika achukue hatua,” amesisitiza.

Katia hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka mkakati wa kukuza zao la mkonge ikiwa ni pamoja na kudhibiti uingizwaji wa bidhaa za nyuzi za plastiki kutoka nje ili kulinda viwanda vinavyozalisha nyuzi za mkonge na kuchochea shughuli za uwekezaji.

Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Korogwe Vijijini, Timotheo Mnzava aliyetaka kujua mkakati gani umewekwa na Serikali kuvutia wawekezaji wa viwanda vya kuchakata zao hilo ili kuwezesha kuwa na masoko ya uhakika.

Amesema Serikali inadhibiti uingizaji wa bidhaa zikiwemo nyuzi zilizotengenezwa kwa plastiki na kuhamasisha matumizi ya nyuzi zilitengenezwa kwa kutumia mkonge ili kumlinda mzalishaji anayetumia zao la mkonge na kuvutia zaidi wawekezaji.

No comments: