ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 15, 2021

WAITARA ATAKA MASLAHI BORA KWA WATUMISHI

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, akisisitiza jambo kwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Sekta ya Uchukuzi (hawapo pichani), alipofunga baraza hilo lililokaa kwa siku mbili kujadili mpango wa bajeti ya sekta hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022, jijini Dodoma.
Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Sekta ya Uchukuzi, wakiimba wimbo wa mshikamano kabla ya Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara (hayupo pichani) kufunga baraza hilo lililokutana kwa siku mbili mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara (katikati waliokaa), akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la Sekta ya Uchukuzi mara ya kufunga baraza hilo lililofanyika jijini Dodoma.

PICHA NA WUU

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, amewataka watendaji wa Sekta ya Uchukuzi na Taasisi zake kuhakikisha wanajali watumishi kwa kusimamia kanuni, taratibu na sheria ili kupata matokeo chanya katika utendaji.

Akizungumza mara baaada ya kufunga Baraza la Wafanyakazi wa Sekta ya Uchukuzi jijini Dodoma, Naibu Waziri huyo amesema ufanisi wa taasisi unakwenda sanjari na kusimamia vizuri maslahi, matumizi bora ya fedha yanayozingatia taratibu, ushirikishwaji na utii kwa Mamlaka.

“Hamuwezi kufanikiwa kama katika taasisi zenu kila mmoja anakwenda njia anayotaka. Lazima mjifunze kuheshimu Mamlaka zilizopo, mjali maslahi ya watumishi, muwashirikishe katika ngazi zote, mkifanya hivyo wala hamtatumia nguvu kusimamia Taasisi na matokeo yataonekana”, amesema Naibu Waziri Waitara.

Naibu Waziri Waitara ameongeza kuwa Serikali imejiwekea malengo ya kukamilisha miradi mikubwa ya kimkakati hivyo ni lazima wakuu wa Taasisi wapate taarifa sahihi za kila siku za maendeleo ya miradi hiyo ili kuwa na kauli moja kuanzia ngazi ya Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wasimamizi.

Aidha, Naibu Waziri Waitara amezitaka taasisi zote zinazokusanya mapato kuhakikisha zinapeleka gawio Serikalini ili fedha hizo zitumike kuendeleza miradi mingine na kutimiza azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwatumikia wananchi kwa kuwapatia miundombinu bora.

Naye, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi Gabriel Migire, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa wataalam wa Sekta wamejipanga kwa kuweka programu maalum ya ukaguzi wa miradi kila mwezi ili kuona maendeleo na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji.

Migire, amesema kuwa sekta iko tayari wakati wote kutoa ushirikiano kwa viongozi kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa weledi kwa kutoa taarifa sahihi hususani kwenye utoaji wa majibu kwa maswali yanayoulizwa bungeni.

Baraza la Wafanyakazi la Sekta ya Uchukuzi limekaa kwa siku mbili ambapo pamoja na mambo mengine limejadili utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2020/21 na mpango wa bajeti kwa mwaka 2021/22.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi

No comments: