ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, April 24, 2021

ZANZIBAR KUUNGANA NA MATAIFA MENGINE KATIKA KUADHIMISHA WIKI YA CHANJO AFRIKA

Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya DK. Fadhil Mohd Abdalla akitoa tarifa ya Wiki ya chanjo Afrika na kumkaribisha Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Nassor Ahmed Mazrui kuzungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Nassor Ahmed Mazrui akiwaeleza waandishi wa habari lengo la wiki ya chanjo Afrika katika mkutano uliofanyika katika Wizara hiyo Mnazimmoja.
Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri wa Afya (hayupo pichani) katika mkutano uliofanyika katika Ukumbi wa Wizara hiyo Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Mratibu wa chanjo Zanzibar Yussuf Haji Makame akitoa utaratibu wa uzinduzi wa wiki ya chanjo Afrika ambao utafanyika katika kituo cha afya Mwera Wilaya ya Magharibi ‘A’ april 27, 2021.
Afisa wa chanjo kutoka Shirika la kuhudumia watoto Duniani (UNICEF) Emannuel Tessua akisisitiza umuhimu wa wasichana wenye umri wa miaka 14 kupata chanjo ya HPV kujikinga saratani ya shingo ya kizazi katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja.

Picha na Makame Mshenga.

Na. Ramadhan Ali Bakari Maelezo Zanzibar

Zanzibar itaungana na Mataifa mengine ya Bara la Afrika katika uzinduzi wa wiki ya Kampeni ya chanjo Afrika itakayoanza tarehe 26 mwezi huu.

Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Mnazimmoja, Waziri wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Nassor Ahmed Mazrui amesema lengo la Kampeni hiyo ni kuongeza msisitizo wa kuwapatia chanjo watoto wote ili kuwakinga na maradhi mbali mbali yanayoweza kuzuilika kupitia chanjo.

Amewataja wahusika wa kampeni ya chanjo Afrika kuwa ni watoto waliofikia umri wa miaka miwili, miaka mitano ambao hawajakamilisha na chanjo ya HPV kwa wasichana wenye umri wa miaka 14.

Waziri Mazrui amesisitiza kuwa chanjo ni mkakati muafaka wa kupunguza maradhi mbali mbali yanayozuilika kwa njia hiyo na kupunguza vifo vya watoto.

Alisema Zanzibar imefanikiwa kwa asilimia 90 kuwaptia chanjo watoto wanaostahiki hata hivyo bado wapo watoto ambao hawajapata kabisa chanjo yoyote hivyo amewataka wazazi na walezi kuitumia fursa ya wiki ya chanjo Afrika kuwapeleka vijana wao kwenye vituo vya kupatiwa chanjo.

Ameizitaja Wilaya za Mjini, Micheweni, Magharibi ‘A’ na Magharibi ‘B’ kuwa hazikufikia lengo lililopangwa na Serikali la kuwapatia chanjo watoto mwaka uliopita 2020

Amewataka viongozi na watendaji wote kuchukua juhudi ya kusimamia Kampeni hiyo kwani kujikinga na maradhi ni kuipunguzia Serikali na familia gharama kubwa za matibabu zisizo za lazima.

Afisa wa chanjo wa Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) Emannuel Tessua alisema Mpango wa Taifa wa chanjo ulianza mwaka 1985 kwa chanjo tano kwa ajili ya kuwakinga watoto na maradhi matano na hadi kufikia mwaka jana kunachanjo tisa zenye uwezo wa kukinga maradhi 13.

Aliyataja maradhi yanayokingwa na chanjo hizo kuwa ni Polio, Suru, Rubela, Pepopunda, Dondakoo, Kifua kikuu, Kuharisha Kichomi, Saratani ya mlango wa kizazi Homa ya Ini na mafua makali.

Hata hivyo Emannuel alisema chanjo ya HPV ya wasichana wenye umri wa miaka 14 kwa ajili ya kuwakingwa na Saratani ya Shingo ya kizazi bado haijawa na mafanikio na ameishauri jamii kutoipuuza chanjo hiyo kwani saratani hiyo inayoongoza kuliko saratani nyengine.

Mratibu wa chanjo Zanzibar Yssuf Haji Makame amewakumbusha wananchi kuwa chanjo zote zinazotolewa na Serikali ni salama na uzinduzi rasmi wa wiki ya chanjo Afrika kwa Zanzibar utafanyika katika kituo cha afya cha Mwera na Waziri wa Afya atakuwa mgeni rasmi.

Kaulimbiu ya Wiki ya chanjo Afrika kwa mwaka 2021 ni ‘Chanjo huiweka jamii pamoja’.

No comments: