Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemuagiza Gavana wa Benki Kuu (BOT), Profesa Florens Luoga kukaa na Wizara ya Fedha na Mipango kujadiliana namna ya kupunguza kiwango cha riba katika mikopo inayotolewa na benki mbalimbali nchini.
Amesema riba kuwa juu ni kikwazo kwa baadhi ya wawekezaji, wafanyabiashara na wananchi wa kipato cha chini kiasi cha kushindwa kukopa katika taasisi hizo za kifedha.
Rais Samia ameyasema hayo jana wakati akifungua jengo la Benki Kuu ya Tanzania Tawi la Mwanza
Pia, amezitaka benki hizo kuanza kutoa mkopo wa muda mrefu ili kuwawezesha wakopaji waanzishe miradi ikiwemo kufungua viwanda, mashamba ya kilimo.
Aidha, ameiagiza BOT kufanya maandalizi kuhusu matumizi ya sarafu za kimtandao, ili mabadiliko hayo yatakapofika nchini, yasiikute nchi haijajiandaa.
“Tumeshuhudia kuibuka kwa safaru mpya kwa njia ya kimtandao, yaani cryptocurrency. Najua bado nchini ikiwemo Tanzania hazijakubali au kuanza kuzitumia safaru hizo. Hata hivyo, wito wangu kwa Benki Kuu ni vyema mkaanza kufanyia kazi maendeleo hayo. Yakija yakitukamata, yasitukamate hatuko tayari,” alisema Rais Samia
Leo tarehe 14 Juni, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan ataendelea na ziara yake mkoani Mwanza kwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Reli ya kisasa yani (SGR) kipande cha tano kutoka Mwanza hadi bandari ya nchi kavu Isaka mkoani Shinyanga, atafanya ukaguzi wa Ujenzi wa daraja la JPM pamoja na ufunguzi wa Mradi wa Maji Misungwi.
No comments:
Post a Comment