WAZIRI
wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amewataka watanzania kuupuuza uzushi
uliojitokeza kutokana na kusambazwa kwa ujumbe wenye taarifa za
kupotosha kuhusu kuingizwa kwa mayai nchini kutokea nchi jirani na
kusababisha soko la mayai yanayozalishwa nchini kushuka bei.
Akizungumza
leo (17.06.2021) ofisini kwake katika Mji wa Serikali Jijini Dodoma,
Waziri Ndaki alisema baada ya kuona ujumbe huo Juni 15 Mwaka huu,
Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilifanya uchunguzi kwenye makao makuu ya mikoa
yote 26 nchini na baadhi ya wilaya ili kujiridhisha juu ya upatikanaji
wa mayai, bei ya trei ya mayai na soko lake kwa ujumla.
Hatua
hiyo inatokana na uwepo wa ujumbe unaozunguka kwenye mitandao ya kijamii
kuhusu kuingia kwa mayai mengi nchini kutoka nje ya nchi kiasi cha
kusababisha kushuka kwa bei ya mayai mpaka kufikia Shilingi 4,000/= kwa
trei.
Ujumbe huo ulikuwa na kichwa cha habari kinachosomeka “SOKO LA MAYAI DSM KITENDAWILI”.
Alisema
njia zilizotumika kukusanya taarifa ni pamoja na kuongea na wafugaji
wakubwa wa kuku wa mayai, wafanyabishara wakubwa na wadogo wa
mayai.Alisema pia walilazimika kufika sehemu za masoko wanakouza mayai
na kujionea hali halisi ikiwa ni pamoja na kujua bei ya trei la mayai,
upatikanaji wake na hali ya soko kwa ujumla.
Waziri huyo alisema
pia walitumia fursa ya kuongea na maafisa mifugo wa mikoa, majiji,
manispaa na halmashauri ili kupata taarifa juu ya bei ya trei la mayai,
upatikanaji wake na hali ya soko la mayai kwenye maeneo yao ya
kiutawala.
Akizungumzia matokeo ya uchunguzi huo, Waziri Ndaki
alisema mayai yanayozalishwa nchini ni kidogo kiasi kwa sababu ya uhaba
wa vifaranga wa kuku wa mayai na tatizo la uhaba wa vifaranga limekuwepo
tangu mwaka 2020 kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID 19 duniani
uliosababisha uingizaji nchini wa vifaranga wa kuku wazazi kupungua
sana.
Alisema hali hiyo imesababisha idadi ya kuku wa mayai
wanaotaga kwa sasa kuwa wachache na kusababisha kuwepo na uhaba wa mayai
nchini huku matokeo zaidi ya uchunguzi yanaonesha kwamba bei ya trei la
mayai katika ngazi ya mfugaji ni kati ya Shilingi 6,500/= mpaka
9,000/=.
“Vilevile bei ya trei la mayai sokoni ni Shilingi
6,800/= katika baadhi ya mikoa mpaka Shilingi 12,000/= kwa mikoa ukiwemo
wa Katavi lakini bei ya yai moja sokoni au madukani ni kati ya Shilingi
250/= mpaka 500/=” Alisema
Alisema mtu aliyezusha taarifa hizi
za uongo ana nia ovu na tasnia ya ufugaji kuku Tanzania na ameleta
taharuki kubwa kwa wafugaji wa kuku na jamii yote ya Tanzania, suala la
uhaba wa vifaranga linafanyiwa kazi na kufikia mwezi wa Septemba, 2021
hali itakuwa imesharudi kama kawaida.
“Wizara inakanusha vikali
taarifa zinazonguka kwenye mitandao ya kijamii kuwa hakuna wingi wa
mayai uliosababisha kushuka kwa bei ya mayai katika ngazi ya mfugaji na
sokoni kinachoonekana zaidi ni kuwa kuna upungufu mkubwa wa mayai nchini
uliosababisha bei kupanda mpaka kufikia Shilingi 12,000/= kwa teri”
Alisema Waziri huyo.
Alisema taarifa zilizosambazwa ni uzushi
mtupu na hazina ukweli wowote kutokana na kwamba serikali ilishazuia
uingizwaji wa kuku na mazao yake kutokana na uwepo wa tishio la ugonjwa
wa mafua makali ya ndege Duniani.
Aidha, Wizara imekuwa ikitoa
vibali maalum vya kuingiza vifaranga na mayai ya kutotolesha ya kuku
wazazi na kumekuwa na matukio machache ya uingizaji wa mayai nchini kwa
njia za panya lakini wizara imekuwa ikidhibiti hali hiyo.
Hata
hivyo alisema mwezi Aprili mwaka huu chama cha wafugaji wa kuku kiliomba
makampuni ya kuku yaruhusiwe kuingiza vifaranga wa kuku wa nyama,
vifaranga wa kuku wa mayai na mayai ya kutotolesha kutokana na uhaba
mkubwa wa vifaranga nchini na serikali imeruhusu kwa kipindi cha miezi
mitatu kuanzia Juni mpaka Agosti 2021 na Tayari makampuni kadhaa
yameshaanza kuingiza nchini vifaranga na mayai ya kutotolesha na hivi
karibuni tatizo hili litafikia ukomo.
Katika hatua nyingine
waziri huyo, akizungumzia hali ya ugonjwa wa homa ya nguruwe na jitihada
zinazochukuliwa kukabiliana na tatizo hilo alisema wizara ilitoa
taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari juu ya kuwepo kwa mlipuko wa
ugonjwa wa homa ya nguruwe (African Swine Fever) katika maeneo ya mikoa
ya Mwanza, Kagera, Shinyanga na Dodoma.
Alisema katika taarifa
yake aliwaagiza wakuu wa Mikoa, wakuu wa Wilaya na wakurugenzi wa
Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa
masharti ya karantini zilizokuwa zimewekwa na wataalamu wa mifugo hasa
kwa vile ugonjwa huo hauna chanjo wala tiba na walisimamia vyema zoezi
hilo.
Aidha alisema wizara imekuwa ikifanya juhudi kubwa
kudhibiti ugonjwa huu na mpaka kufikia mwishoni mwa Mwezi Aprili, 2021
sehemu nyingi za nchi hakukuwa na matukio ya ugonjwa huo.
“Mnamo
tarehe 01/06/2021 katika Manispaa ya Morogoro kulijitokeza matukio ya
nguruwe 14 kufa na uchunguzi wa kimaabara ulionesha ugonjwa wa homa ya
nguruwe “Alisema
Alieleza kwamba tayari juhudi kubwa za
kuudhibiti zinaendelea ambazo ni pamoja na kuweka zuio (karantini) ya
kuingiza na kutoa nguruwe na mazao yake katika Manispaa ya Morogoro
tangu tarehe 03/06/2021 na elimu kwa wafugaji na wadau wengine wa
nguruwe njia za kukinga ugonjwa usiingie kwenye mabanda ya nguruwe.
Alieleza
kwamba mpaka kufikia tarehe 17/06/2021 hali ya ugonjwa katika Manispaa
ya Morogoro ulikuwa umedhibitiwa na hakuna kifo tena kilichotokea kwa
nguruwe.Hata hivyo alisema Juni 9 mwaka huu wizara ilipata taarifa juu
ya uwepo wa ugonjwa wa homa ya nguruwe katika Jiji la Dar es Salaam.
Alisema
baada ya kufanya uchunguzi katika mashamba ya nguruwe, ilibainika
kuwepo kwa taarifa za nguruwe 298 kufa katika mashamba mawili kwa kile
kilichodhaniwa ni ugonjwa wa homa ya nguruwe.
Alieleza baada ya
kuchunguza kwa kina kwa wanyama waliokuwa wamebaki kwenye mashamba hayo
pamoja na kuchukua sampuli na kuzipima katika maabara, ilibainika kuwa
ilikuwa sio ugonjwa wa homa ya nguruwe.
Aliongeza kwamba
ufuatiliaji zaidi ulifanyika kwenye sehemu zote za machinjio ya nguruwe
Dar es Salaam na kuchunguza nguruwe wanaochinjwa, hapakuwa na viashiria
vyovyote vya ugonjwa wa homa ya nguruwe.Wizara kwa kushirikiana na wadau
wa maendeleo inaendelea na juhudi za kudhibiti kabisa ugonjwa huu
nchini.
No comments:
Post a Comment