Na, Josephine Majura, WFM, Dodoma
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya Mawaziri wa Sekta mbalimbali na kuwahakikishia kuwa maeneo yote ya kipaumbele yatazingatiwa ili kuchochea maendeleo ya nchi kupitia miradi itakayotekelezwa na Wizara hizo.
Dkt. Nchemba alisema kuwa lengo la kikao hicho lilikuwa ni kujadili na kupitia maeneo ya vipaumbele kwenye kila sekta ili kuona kama yamejumuishwa kwenye hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kabla ya kusomwa Bungeni Jijini Dodoma Juni 10 mwaka huu.
“Nimekutana na viongozi mbalimbali ili kupunguza mazingira yaliyokuwa yakijitokeza nyuma kwamba maeneo ya vipaumbele vya Sekta fulani hayajawekwa sawa”, Alisema Dkt. Nchemba.
Aliongeza kuwa maeneo mengi ya vipaumbele yamekuwa yakiwekwa tofauti na matakwa ya Wizara na Sekta husika hivyo kikao hicho kilikaa ili kubainisha maeneo ya vipaumbele ambayo hayakujumuishwa kwenye Bajeti Kuu na kuangalia uwezekano wa kuyajumuisha kama ilivyopendekezwa.
Mhe. Dkt. Nchemba alieleza kuwa kikao hicho kimejikita katika kujadili mapendekezo ambayo yaliyopo katika hotuba ya Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan pamoja na mipango na dira ya maendeleo ya uchumi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Mhe. Geoffrey Mwambe amepongeza hatua hiyo kwani italeta tija kwa kuwa kila sekta imepata nafasi ya kutoa maoni kwa lengo la kuboresha.
“Nampongeza Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu kwa kuitisha kikao hiki ni utaratibu mzuri sana na unatakiwa kuwa endelevu ili kuleta matokeo chanya”, alisisitiza Mhe. Mwambe.
Aliongeza kuwa katika kikao hicho wameweza kufanya mapitio ya kodi mbalimbali kwa ajili ya kuzifanyia maboresho ili ziwe rafiki kwa wananchi na kuwafanya waweze kulipa kwa hiyari.
Aidha Mhe. Mwambe alisema kuwa kodi zikiwa rafiki kwa wawekezaji na wafanyabiashara wataweza kulipa kwa wakati na kodi hizo zitaisaidia Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kikao hicho cha Mawaziri wa Sekta kimefanyika ofisi ya Waziri wa Fedha na Mipango Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Mawaziri mbalimbali wa Wizara 9 ikiwemo Viwanda na Biashara, Kilimo, Mifugo, Maliasili na Utalii, Afya, Ardhi, TAMISEMI, Uwekezaji na Wizara ya Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment