ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 1, 2021

Jambazi Sugu Auwa Wakati Akijaribu Kuwatoroka Polisi Shinyanga

 


SALVATORY NTANDU
Mkazi wa mtaa wa Ndembezi manispaa ya Shinyanga anayetuhumiwa kuwa ni jambazi sugu, Idd Masasi (43) ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi katika tukio la  majibizano ya risasi wakati akijaribu kuwatoroka polisi baada ya kukataa kujisalimisha kwa vyombo vya usalama.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani humo,kamishina msaidizi wa jeshi la polisi (ACP) Debora Magiligimba amethibitisha kutokea kwa tukio hilo  mei 31 mwaka huu na kusema kuwa Idd anatuhumiwa kufanya matukio ya uhalifu ya unyang’anyi wa kutumia silaha katika mikoa ya Shinyanga na Dar es salaam.

“Jeshi hilo lilipata taarifa za siri za uwepo wa jambazi (Idd Masasi) ambaye alikuwa anatafutwa na jeshi la polisi  makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha hasa matukio yaliyotokea hivi karibuni katika maeneo ya kigamboni na Dar es salaam na kisha kukimbilia mkoani Shinyanga,”alisema Magiligimba.

Alisema kuwa taarifa za kutafutwa kwake zilifunguliwa katika vituo vya Polisi kigamboni kwa kumbumbu za vitabu namba  KGD/IR/1050/2021, KGD/IR/411/2021 ambazo zilifunguliwa kwa lengo la kuendelea kumtafuta ili aweze kufikishwa kwa vyombo vya ulinzi na usalama baada kutoroka baada ya kutekeleza uhalifu huo.

“Baada ya kupata taarifa askari wetu  wakishirikiana na kikosi kazi cha askari kutoka jijini Dar es Salaam liliweka mtego maeneo ya soko la Nguzo Nane na ambapo majira ya saa tano alipofika katika eneo hilo na aligundua anafuatiliwa  alianza kukimbia ndipo askari walipompa ilani ya kusimama kwa kufyatua risasi hewani lakini alikaidi,”alisema Magiligimba

Kamanda Magiligimba amesema kuwa askari waliamua kumfyatulia risasi mbili bila kuleta madhara kwa watu wengine waliokuwepo eneo hilo, risasi hizo zilimjeruhi mguu wa kushoto na sehemu ya mgongoni na kisha  kumkamata na kupelekwa hospitali ya mkoa kwajili ya matibabu na alifariki dunia wakati anapatiwa matibabu.

“Nitoe onyo kwa waharifu wote kuwa mkoa wetu siyo sehemu rafiki ya kutenda uharifu au kukimbilia waharifu kujificha baada ya kufanya uharifu mikoa mingine kwani jeshi la polisi limejipanga vizuri kukabiliana nao, aidha mharifu yeyote atakayethubutu kufanya uharifu atakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, waharifu wote wafahamu kwamba sehemu ambayo wapo na sisi jeshi la polisi tupo,” alisema Magiligimba

Kamanda Magiligimba amefafanua kuwa kumbukumbu za polisi zinaonyesha kuwa Idd alishawahi kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha mwaka 2011 na kutumikia adhabu hiyo katika gereza la Butimba, Mwanza na baadae alitoka kwa rufaa.

Mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitalini hapo kwa ajili ya uchunguzi.

No comments: