ANGALIA LIVE NEWS

Friday, July 30, 2021

AJITEKA, AKICHOMA ILI ATUMIWE MILLIONI 3

JESHI la Polisi Mkoa wa Arusha linamshikilia kijana mmoja Dickson Peter Mungulu kwa kosa la kutoa taarifa za uongo kuwa ametekwa na kutaka ndugu zake wamtumie shilingi Milioni tatu ili aachiwe.

Inaelezwa kuwa kijana huyo amekutwa na majeraha sehemu ya shingo na mguu ambapo amekiri kujichoma na kitu chenye ncha kali yeye mwenyewe kwa nia ya kuaminisha wazazi wake pamoja na ndugu zake wengine kwamba alitekwa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha ACP Justine Masejo amesema kuwa tukio hilo limetokea Julai 25, 2021.

“Siku ya tukio muda wa saa saa 9 na dakika 20 Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha lilipokea taarifa kutoka kwa mtu mmoja (jina limehifadhiwa) kuwa ndugu yake aitwaye Dickson Peter Mungulu ametekwa ambapo taarifa hizo walizipata kupitia ujumbe mfupi wa simu (SMS) uliotumwa kutoka kwa simu ya mhanga ukieleza kwamba ametekwa na ili aachiwe zinahitajika kiasi cha fedha Shilingi Milioni Tatu (Tsh.3,000,000) vinginevyo atauawa”,ameeleza Kamanda Masajo.

Amesema kuwa baada ya kupokea taarifa hizo Jeshi la Polisi mkoani Arusha lilifanya uchunguzi wa kina na tarehe 28.07.2021 muda wa jioni Jeshi la Polisi lilifanikiwa kumpata kijana huyo aliyesadikika kuwa ametekwa huko maeneo ya Morombo katika nyumba ya kulala wageni (Jina limehifadhiwa).

Kamanda wa Polisi amesema kuwa baada ya kumhoji Dickson Peter Mungulu ambaye mwaka 2020 alimaliza Shahada ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Makumira kilichopo Arusha, ilibainika kuwa alitoa taarifa za uongo kwa ndugu zake ili pate kiasi hicho cha fedha ziweze kumsaidia kulipa madeni yake mbalimbali yanayomkabili.

ACP Masejo amesema kuwa sambamba na hilo baada ya kumchunguza zaidi katika mwili wake ilibainika kuwepo na majeraha sehemu ya shingo na mguu alikiri kujichoma na kitu chenye ncha kali yeye mwenyewe kwa nia ya kuuaminisha wazazi wake pamoja na ndugu zake wengine kwamba alitekwa.

Jeshi la Polisi Mkoani Arusha linaendelea na upelelezi wa tukio hilo na pindi utakapokamilika jalada litapelekwa Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali kwa hatua zaidi za kisheria.

Kamanda Masejo ametoa wito kwa wananchi,vijana wenye tabia kama hiyo ilionyeshwa na kijina huyo kuwa, Jeshi la Polisi halitawafumbia macho wale wote watakao husika na litawachukuliwa hatua kali za kisheria kwa wataobainika kupotosha umma na kutoa taarifa za uzushi kwa kwa jamii.

“Pia niwaombe wananchi kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu katika maeneo yao kwa Jeshi la Polisi ili zifanyiwe kazi,” ameongeza.

Habari kwa hisani ya GPL

No comments: