Mratibu wa Ugonjwa wa Homa ya ini kutoka Wizara ya Afya Dkt. Baraka Nzobo akizungumza na Waandishi wa habari (Hawapo Pichani) leo Julai 28,2021 jijini Dodoma wakati akisoma Tamko la SIku ya Maadhimisho ya ya Siku ya Homa ya Ini Duniani kwa niaba ya Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima.
UGONJWA wa Homa ya Ini umetajwa kuwa wa hatari na unaoua idadi kubwa ya watu polepole ambapo kati ya watu 100 nane wanaweza kuwa na maambukizi sugu ya ugonjwa huo.
Kutokana na hali hiyo, Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, imechukua hatua mbalimbali kudhibiti ugonjwa huo ikiwemo kuanzisha huduma ya kinga ya maambukizi ya homa ya ini kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto.
Akitoa tamko la kilele cha maadhimisho ya siku ya Homa ya Ini duniani,leo Julai 28,2021,jijini Dodoma Waziri wa Afya,Dkt.Doroth Gwajima amesema ugonjwa wa Homa ya Ini ni tatizo linalohitaji juhudi za dhati kupambana nalo.
Amesema ugonjwa huo umetajwa kuwa wa hatari na unaoua idadi kubwa ya watu polepole ambapo kati ya watu 100 nane wanaweza kuwa na maambukizi sugu ya ugonjwa huo.
“Na wanaweza wasioneshe dalili zozote na kwamba asilimia kubwa ya wagonjwa huugundua ugonjwa huu kwenye hatua za mwisho na hivyo kushindwa kupata matibabu mapema na kupelekea mgonjwa kupoteza maisha,”amesema.
Waziri Gwajima amesema maambukizi ya ugonjwa huo kusababishwa na virusi ambavyo vinapoingia mwilini mwa binadamu hushambulia ini na hivyo kulifanya wakati mwingine lisinyae na kushindwa kufanya kazi vizuri.
Amesema katika hatua za mwisho mwathirika wa ugonjwa huo anaweza kupata saratani ya ini ambapo amedai ugonjwa huo unaenezwa kwa njia mbalimbali kulingana na kundi la virusi hivyo.
Waziri Gwajima amesema virusi vya homa ya Ini vipo katika makundi matano ambayo ni A,B,C,D na E.
“Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa watu 884,000 hufariki kila mwaka kutokana na matatizo yanayotokana na homa ya ini hasa saratani ya ini.Inakadiriwa kuwa kila baada ya dakika mbili watu wawili hufariki kutokana na homa ya ini duniani,”amesema.
Amesema ugonjwa huo unaweza kukingwa kwa kutumia chanjo ambayo hutolewa kwa mtu asiye na maambukizi ya virusi hivyo.
“Kwa maambukizi ya kirusi aina ya B chanjo ya ugonjwa huo hutolewa kwa mtu asiye maambukizi ya virusi hivyo kutoa kinga kwa kipindi chote cha maisha yake.Hivyo niwasisitizie wananchi kwenda kufanyiwa uchunguzi wa homa ya ini,”amesema.
Amesema Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kudhibiti ugonjwa huo kwa kusimamia mpango Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti na kutokomeza ugonjwa huo wa mwaka 2018-2023.
Pia,kuandaa vielelezo vinavyohusu ugonjwa huo ili kuelimisha umma juu ya ugonjwa huo na namna gani maambukizi yanaweza kuzuiwa.
Vilevile, kuendelea kutoa chanjo ya hepatitis B kwa watumishi wa afya walio katika mazingira hatarishi pamoja na kuanzisha huduma ya kinga ya maambukizi ya homa ya ini kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto.
Ametaja mikoa iliyokuwa na maambukizi makubwa ya homa ya Ini kwa mwaka 2020 kwenye kundi la watu wanaochangia damu ni Mara asilimia 9.3, Geita asilimia 8.7, Morogoro asilimia 7.7, Rukwa asilimia 7.6 na Shinyanga ni asilimia 7.4.
Aidha Dk.Gwajima amewataka wananchi kufanya uchunguzi wa homa hiyo na watakaobainika kuwa na maambukizi watapatiwa chanjo hiyo kwa gharama nafuu kwenye hospitali za serikali.
Pia Waziri ameziataka hospitali binafsi na za mashirika ya kidini kushusha gharama za upimaji na utoaji wa chanjo ili kuwafikia wananchi wote.
Akitoa semina kwa waandishi kuhusu ugonjwa huo,Mratibu wa homa ya Ini kutoka Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii ,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Baraka Nzobo amewahimiza akina mama wajawazito kuhakikisha wanapimwa homa ya Ini pindi wanapohudhuria
kliniki ili kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kujifungua.
Amesema kuwa,wakati wa mahudhurio ya kliniki kwa mama wajawazito anapofikisha miezi saba ya ujauzito anapaswa kupewa dawa ili kupunguza nafasi kubwa ya motto kuzaliwa na maambukizi ya virus vya homa ya ini
“Mama anaweza kumwambukiza mtoto wakati wa kujifungua ,sasa tunahimiza akina mama wajawazito wapimwe ,na akina mama hao katika miezi saba hupewa dawa ili kupunguza ‘chance’ya mtoto kuzaliwa na virus hivyo.”amesema Dkt.Nzobo
No comments:
Post a Comment