Wananchi wa kata ya Makowo halmashauri ya mji wa Njombe mkoani Njombe wameiomba wizara ya afya kuwapatia vifaa tiba na wataalamu wa afya ili wafungue kituo chao cha afya walichojenga kwa kushirikiana na serikali ili kuondoa adha kubwa ya upatikanaji wa huduma za afya hususani akina mama wajawazito.
Taarifa ya ujenzi wa kituo hicho cha afya iliyosomwa na kaimu afisa mtendaji wa kata ya makowo Erick Mkonga katika ziara ya kibunge ya mbunge wa jimbo la Njombe mjini imeeleza kuwa zaidi ya shilingi milioni 510.86 zimetumika ambapo wananchi wamechangia zaidi ya shilingi milioni 40 lakini hadi sasa bado hakijafunguliwa wakisubiri serikali kuwasaidia.
“Jumla ya mapato yote katika mradi huu wa kituo cha afya,ni shilingi milioni mia tano na kumi laki nane stini elfu.Fedha hii imetokana na mapato ya ndani,mfuko wa jimbo”alisema Erick Mkongwa
Mganga mkuu wa halmashauri ya mji wa Njombe dokta Isaya Mwasubila amesema hadi sasa zimesalia asilimia 10 pekee ili kituo hicho kiweze kufunguliwa kwani wananchi wametekeleza wajibu wao kwa asilimia 100.
“Changamoto kubwa ni watumishi na vifaa tiba kwasababu kazi iliyosalia ni asilimia 10 tu na hela za kumalizia zipo ameshazileta mkurugenzi”alisema Isaya Mwasubila
Akihutubia mamia ya wakazi wa Makowo baada ya kutembelea na kukagua kituo hicho cha afya mbunge wa jimbo la Mjombe mjini Deo Mwanyika amesema kazi kubwa iliyofanywa na wananchi hao zinapaswa kuungwa mkono kwa serikali kuwasaidia upatikanaji wa vifaa tiba na wataalamu na kwamba ataendelea kufuatilia wizarani hadi wafanikiwe.
“Tutahakikisha tunamleta waziri hapa ili aweze kuangalia kituo chetu na ninaamini kwa sala za wananchi tutafanikiwa juu ya hiki kituo”alisema Deo Mwanyika
Naye diwani wa kata ya Makowo Honoratus Mgaya amesema “Sisi wana Makowo tunaomba vifaa tiba na pili tunaomba waganaga Makowo”
Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Makowo akiwemo Lusinus Mwalongo,Yasinta Msemwa na Emilian Mwalongo wamesema endapo serikali itawasaidia kufunguliwa kwa kituo hicho basi wataepukana na adha ya kutumia gharama kubwa kwenda kutafuta huduma za afya umbali mrefu kwenye hospitali za Ikonda wilayani Makete na Kibena mjini Njombe kwa kuwa zahanati yao wanayoitumia haina uwezo wa kutoa baadhi ya huduma muhimu.
No comments:
Post a Comment