ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 19, 2021

WATU NANE WAKIWEMO WATUMISHI WATATU WA SERIKALI WAKAMATWA WAKIWA NA DAWA ZA KULEVYA

Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na dawa za Kulevya, Kamishna Jenerali Gerald Kusaya akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Jijini Dar es Salaam.

PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na dawa za Kulevya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wamefanikiwa kukamata dawa za kulevya Kilo 99.33 mwezi Juni mwaka huu katika matukio tofauti zikihusisha watu nane kati yao watatu wakiwa ni watumishi wa Serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam,akitoa taarifa hiyo Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na dawa za Kulevya, Kamishna Jenerali Gerald Kusaya amesema kuwa tarehe 19 Juni mwaka huu katika eneo la Bunju Beach walimkamata aliyekuwa askari Polisi F.6763 CPL Deodatus Leonid Massare (37) kabila Marangi akiwa na kilo 1.04 ya dawa za kulevya aina ya heroin.

“Juni 21, mwaka huu katika maeneo ya Mivinjeni Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam, tulimkamata Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Andrew Wailes Paul (45) kabila Muha, mkazi wa Kurasini na wenzake Said Rashid Mgoha (45) maarufu kama Kindimu kazi yake fundi gereji kabila Mkwere mkazi wa Mtoni Kijichi, na mwinine George David Mwakang’ata (38) kabila Mnyakyusa, Mfanyabiashara Mkazi wa Mtoni Kijichi, wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin kiasi cha kilo 1.02”. Amesema Kamishna Jenerali Kusaya.

Aidha tarehe 18 Juni mwaka huu katika eneo la Mburahati Madoto NHC Wilaya ya Ilala mkoani Dar es Salaam, walifanikiwa kuwakamata mume na mke ambao ni Jamal Said Nangatukile (45) kabila Mmakonde na Mariyamu Rashid Bacha (28) kabila Mburushi wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroin yenye uzito wa gramu 494.52.

” Juni 23,mwaka huu pia walimkamata Afisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania Ally Juma Ally (32) kabila Mzaramo, mkazi wa Kinyerezi pamoja na Abubakar Juma Abdall (28)mkabila Mshiraz, mfanyabiashara wakiwa na dawa za kulevya aina ya methamphetamine yevye uzito wa gramu 597.61. Aidha, katika upekuzi uliofanyika nyumbani kwa Ally maeneo ya Zimbili Kinyerezi, kulipatikana pesa taslimu Tsh.82,043,000 na USD 5100″. Amesema Kamishna Jenerali Kusaya.

Hata hivyo amesema watuhumiwa wote wameshafikishwa mahakamani wakikabiliwa na makosa ya kujihusisha na usafirishaji na biashara ya dawa za kulevya makosa mabayo ni uhujumu Uchumi kwa sheria za nchi yetu.

No comments: