ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, October 7, 2021

SERIKALI HAITOWAVUMILIA WATUMISHI WA UMMA WATAKAOSHINDWA KUTIMIZA WAJIBU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mtakatifu Martin ya Kipatimu wilayani Kilwa, Dkt. Christina Kasyama (kulia) kuhusu mashine ya X-ray wakati alipotembelea hospitali hiyo
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wauguzi wa Hospitali ya Mtakatifu Martin ya Kipatimu wilayani Kilwa wakati alipoitembelea, Oktoba 6, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan haitawavumilia watumishi wa umma watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

“…Rais anahitaji kuona watumishi wa umma wakifanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia maadili. Pia anataka kuona watumishi wakiwafuata wananchi katika maeneo yao ya makazi na kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.”

Ameyasema hayo leo (Jumatano, Oktoba 6, 2021) wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Kipatimu wilayani Kilwa baada ya kutembelea Hosptali ya Mission ya Kipatimu akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani Lindi.

Mheshimiwa Majaliwa amewataka watumishi hao wahakikishe wanatekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi kwa kufuata taratibu zilizowekwa pamoja na kusimamia vizuri fedha za miradi ya maendeleo zinazopelekwa katika maeneo yao.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Dkt. Kheri Kagya ahakikishe mtaalamu wa X-ray anapelekwa katika Hosptali ya Mtakatifu Martin iliyopo Kipatimu ili kuwapunguzia wananchi wa maeneo hayo kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Ametoa agizo hilo baada ya uongozi wa hospitali hiyo ambayo inaendeshwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Kanisa Katoliki kumueleza Waziri Mkuu kwamba hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa mtaalamu wa X-ray licha ya kuwa na kifaa hicho.

Pia, Waziri Mkuu amemuagiza Dkt. Kagya ahakikishe hospitali hiyo ambayo kwa sasa ina daktari mmoja iongezewe daktari mwingine ili kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi.

Awali, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Christina Kasyama alisema hospitali hiyo ambayo inamilikiwa na Jimbo Katoliki la Lindi inafanya kazi kwa ushirikiano na Serikali kupitia mkataba wa huduma (PPP) na inahudumia wakazi takribani 50,000 wa Kilwa Kaskazini na maeneo ya jirani.

No comments: