WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa, wataalam wetu wa afya na elimu na wengine wote walioshiriki katika hafla ya uelimishaji jamii kuhusu Usonji, kutumia elimu hiyo waliopata kuwaelimisha wengine.
Dkt. Gwajima amesema hayo wakati akifungua hafla ya uelimishaji jamii kuhusu Usonji, uliyoambatana na uchangishaji fedha kwaajili ya kuwawezesha vijana wenye usonji kupata mafunzo ya kilimo mahiri yaliyoandaliwa na Lukiza Autism Foundation, Jijini Dar es Salaam.
“Nitoe rai kwa wataalam wetu wa afya na elimu au wawakilishi wao, madaktari, Ustawi wa jamii, walimu wa watoto wenye uhitaji maalum, waandishi wa habari na wengine wote mlioshiriki katika hafla hii, kutumia elimu na uelewa uliopatikana leo kuwaelimisha wengine” Amesema Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima amesema kwa mujibu wa Takwimu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2020 zinaonesha kuwa katika kila watoto 132 Duniani, mtoto mmoja ana Usonji.
“Tanzania, takwimu zilizopo ni za idadi ya Watoto wenye usonji waliofanyiwa usaili katika shule maalum na wale walioonwa katika vituo vya kutolea huduma. Takwimu za mwaka 2018 zinaonesha kuwa, wanafunzi 1416 wana Usonji na walimu 157 katika shule 18 za Msingi”, ameeleza Waziri Gwajima.
Aidha, Dkt.Gwajima ametoa rai kwa wataalam wa afya na elimu wakiwemo madaktari, Ustawi wa jamii, walimu wa watoto wenye uhitaji maalum, waandishi wa habari na wengine wote waliopata fursa ya kushiriki katika hafla ya elimu ya Usonji, kutumia ujuzi huo kuwaelimisha wengine ili kuepuka unyanyapaa dhidi ya watu wenye changamoto hiyo.
Pia katika hatua nyingine Dkt Gwajima amewataka washiriki wa hafla hiyo ya Elimu ya Usonji kuyafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa katika hafla huyo ili kuona tunaishi kwa upendo na bila kuwabagua na kuwanyanyapaa watu wenye tatizo la Usonji.
Dkt. Gwajima ametoa wito kwa Taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Kiserikali kufanya tafiti kuhusu tatizo la usonji, na kuweka wazi kuwa, Serikali itatoa ushirikiano kuhakikisha kuwa tafiti hizi zinafanyika na matokeo ya tafiti hizo yanatumika kuimarisha huduma kwa watoto wenye Usonji nchini.
“Ninatoa wito na kuhimiza Taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Kiserikali kufanya tafiti kuhusu tatizo la usonji na serikali itatoa ushirikiano kuhakikisha kuwa tafiti hizi zinafanyika na matokeo ya tafiti hizo yanatumika kuimarisha huduma kwa watoto wenye Usonji”, ameeleza Waziri Gwajima.
No comments:
Post a Comment