Advertisements

Friday, July 8, 2022

RAIS SAMIA KUFUNGUA MKUTANO WA 65 WA KIMATAIFA UNWTO JIJINI ARUSHA

  

Waziri wa Utalii, Dr Pindi Chana Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano huo


Na Jane Edward, Arusha
Rais Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kufungua mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO), unaowahusisha Mawaziri wa Utalii Afrika pamoja na mambo mengine, watajadili uwekezaji kwa ajili ya kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini.

Mkutano huo, utakaohudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa UNWTO, unalenga kujenga upya ustahimilivu wa utalii Barani Afrika, kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Akizungumzia mkutano huo wa utalii wa mikutano utakaofanyika Jijini Arusha, Oktoba 5 hadi 7, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana, alisema miongoni mwa watu mashuhuri watakaohidhuria mkutano huo ni Katibu Mkuu wa UNWTO.

Balozi Dk. Chana, alisema mkutano huo ni mojawapo ya hatua za kimkakati za kukuza na kuendeleza sekta ya utalii nchini pamoja na kuendelea kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania Kimataifa pamoja na fursa za uwekezaji.

"Katika mkutano huo, Mawaziri wa Utalii kutoka nchi wanachama wa Shirika la UNWTO, Kamisheni ya Afrika na wadau wa utalii kutoka ndani na nje ya Afrika watashiriki.

"Mkutano huo utahusisha matukio mbalimbali ikiwemo Jukwaa la Uwekezaji, kwa ajili ya kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini."

Aidha, Waziri Balozi, Dk. Chana alisema katika mkutano huo, kutatolewa mafunzo ya market symposium (mafunzo kwa wadau wa sekta ya utalii) ili kuwajengea uwezo wadau wa utalii kuhusu utangazaji utalii.

Vilevile, Waziri huyo amefafanua kuwa, pia wafanyabiashara za utalii pamoja na wadau wengine wa sekta hiyo watapata fursa ya kutangaza biashara zao kupitia matukio yatakayoambatana  na mkutano huo wa Kimataifa wa kwanza kufanyika Tanzania.

"Kimsingi mkutano huo utatochea ukuaji wa zao la utalii wa mikutano na matukio kama ilivyoainishwa katika ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2020 na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka mitano, awamu ya tatu (2021/22)-2025/26 kwa lengo la kufikia watalii milioni tano na mapato ya Dola za Marekani, bilioni sita ifikapo mwaka 2025,"alisisitiza 

Kwa mujibu wa Waziri huyo, ongezeko la idadi ya watalii wa kimataifa wanaotembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini, limefikia watalii 458,048.

Katika mkutano huo na Waandishi wa Habari, Mkurugenzi wa Kamisheni ya Afrika ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia utalii (UNWTO), Marie-Alise Grandcourt, alisema anaridhishwa na maandalizi ya mkutano huo yanayofanywa na serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye sasa ni kinara wa kutangaza fursa za utalii za nchi yake.

Mkurugenzi huyo, aliambatana na Naibu Mkurugenzi wa UNWTO, Kamisheni ya Afrika, Jaime Mayaki.

No comments: