Na. Mwandishi wetu Jeshi la Polisi.
Katika kuhakikisha wimbi la ajali za barabarani zinapungua kama sio kumalizika kabisa Jeshi la Polisi Mkoani Arusha kwa kushirikiana na Chuo cha Ufundi Arusha limetoa mafunzo ya udereva kwa Askari Polisi zaidi ya 100.
Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoani humo Mrakibu Mwandamizi wa Polisi SSP Zauda Mohamed wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo leo amesema lengo ni kuwajengea weledi madereva hao pindi wanapotumia vyombo vya moto barabarani ikiwa ni utekelezaji wa kauli mbiu ya Jeshi hilo ambayo ni Nidhamu, Haki, Weledi na Uadilifu.
SSP Zauda amebainisha kuwa mafunzo yaliyotolewa yatasaidia madereva wa Polisi kuwa na nidhamu wakati wakiendesha vyombo hivyo huku akifafanua kuwa mafunzo hayo ni endelevu na yatafanyika kwa madereva wengine wa Vyombo vya usalama.
Aidha Mkuu huyo wa usalama barabarani amesema kuwa mbali na madereva wa vyombo vya usalama pia mafunzo hayo yanaendelea kutolewa kwa madereva wa magari ya Utalii, abiria na yale ya mizigo ndani na nje ya Mkoa huo.
Kwa upande wake Mwanasheria wa Kikosi cha Usalama barabarani Mrakibu wa Polisi SP Deus Sokoni amesema madereva wa Serikali wamekua wakisababisha ajali nyingi za barabarani hivyo kutoa msukumo kwa taasisi mbalimbali hususani Jeshi la Polisi kuanzisha mafunzo hayo.
SP Sokoni pamoja na kumshukuru Mkuu wa Usalama barabarani mkoani humo kwa kuanzisha mafunzo hayo pia amewataka madereva wote waliopatiwa mafunzo hayo kuwa mabalozi wazuri wa kusimamia na kufuata sheria za usalama barabarani.
Naye Bwana David Mtunguje ambaye ni mkufunzi wa chuo hicho alibainisha kuwa jumla ya madereva 103 walipatiwa mafunzo ambapo walifundishwa sheria za barabarani, alama za barabarani pamoja na kulijua gari.
Bwana Mtunguje amesema kupitia mafunzo hayo ajali nyingi za barabarani zitaenda kupungua kwa sababu asilimia 76 kwa sababu nyingi zinasababishwa na uzembe wa madereva.
Kwa upande wa Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Mnaku Msabila ambaye ni mnufaika wa mafunzo yaliyotolea mbali na kushukuru kwa ujuzi aliopatiwa ameshauri pia mafunzo hayo yawe endelevu kwa askari wengine ili wapate utaalamu na ujuzi wa kutosha.
Mafunzo hayo yanaendelea kutolewa ikiwa ni mkakati wa Jeshi hilo la kuhakikisha linapunguza ama kumaliza ajali za barabarani mkoani humo hasa ikizingatia ni kitovu cha Utalii nchini.
No comments:
Post a Comment