ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 15, 2023

DKT. JAFO: WANANCHI WAPANDE MITI



Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi wananchi hawana budi kushiriki katika zoezi la upandaji wa miti.

Amesema hayo leo Juni 15, 2023 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu maswali ya wabunge wa Viti Maalumu Mhe. Mariamu Kisangi na Mhe. Jacqueline Msongozi waliouliza mikakati ya Serikali ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Jafo amesema kuwa kwa mujibu wa wataalamu wa hali ya hewa kiwango cha mvua kimeshuka kutokana na changamoto hiyo na kusababisha ukame katika baadhi ya maeneo yakiwemo mikoa ya Arusha na Manyara.

Hivyo, Serikali imeelekeza kila halmashauri kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka na kuitunza ikiwa ni hatua ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Awali Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema amewahamasisha wananchi kuacha shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira ambazo husababisha mabadiliko ya tabianchi.

Amewaasa wananchi kuacha kukata miti ovyo, kuepuka kilimo kisicho endelevu katika vyanzo vya maji, kuepuka ufugaji unaoharibu mazingira pamoja na uvuvi haramu.

Naibu Waziri Khamis amesema kuwa Serikali inachukua hatua kwa kuanzisha na kutekeleza miradi ya kuzuia madhara ya mabadiliko ya tabianchi katika jamii.

Aidha, amesema kuwa Serikali imeandaa Sera, Mikakati na Mipango ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ambayo inatoa elimu na namna bora ya kukabiliana na athari hizo kwa wadau wote muhimu wakiwemo wananchi katika maeneo yote nchini.


No comments: