ANGALIA LIVE NEWS

Friday, June 9, 2023

RAIS SAMIA AITAKA TNBC KUIMARISHA UWEZO WA SEKTA BINAFSI NCHINI


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara  (TNBC) akizungumza na viongozi mbalimbali pamoja na wafanyabiashara wakati akifungua Mkutano wa 14 wa Baraza hilo Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Juni, 2023.

Viongozi mbalimbali, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wafanyabiashara wakiwa kwenye mkutano wa 14 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) uliofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Juni, 2023.

Rais za Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi akiwa kwenye Mkutano wa 14 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Juni, 2023

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara  (TNBC) akishiriki kwenye Mkutano wa 14 wa Baraza hilo Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 09 Juni, 2023.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji kupitia Sera, Sheria na Taratibu kumewezesha kuongezeka kwa pato la taifa kutoka trilioni 39.9 mwaka 2021 hadi trilioni 45.2 mwaka 2022.

Rais Samia amesema hayo leo wakati akifungua Mkutano wa 14 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete, Ikulu- Magogoni.

Aidha, Rais Samia amesema TNBC itaendelea kuwa moja ya vyombo rasmi vya kuishauri Serikali kuhusu hatua muhimu za kuimarisha biashara kwa lengo la kujenga uchumi shirikishi.

Rais Samia pia ameihimiza TNBC kufanya mashauriano ambayo yataimarisha uwezo wa sekta binafsi nchini kuzalisha bidhaa za huduma zitakazopunguza uagizaji na kuongeza mauzo katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Vile vile, Rais Samia amesema hatua hiyo itaiwezesha Tanzania kupunguza matumizi ya fedha za kigeni, kuongeza mapato na hivyo kuimarisha uchumi wa nchi.

Kwa upande mwingine, Rais Samia amewaagiza viongozi katika ngazi zote kuendeleza majadiliano kupitia Mabaraza ya Biashara ya ngazi za mikoa na wilaya ili kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji.

Hali kadhalika, Rais Samia amesema Serikali inaendeela kuweka mkazo katika kutekeleza miradi ya kimkakati ikiwemo ya miundombinu, nishati na TEHAMA ambayo inawezesha kukua kwa biashara.

No comments: