ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 20, 2023

VIONGOZI WAPYA RITA WAANZA KAZI


Kabidhi Wasii Mkuu na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA) Bw. Frank Kanyusi amewataka watumishi wa Wakala hiyo kufanya kazi kwa ushirikiano, umoja na upendo ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao na kuwawezesha kutoa huduma bora kwa wananchi wananowahudumia kote nchini.
Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki Jijini Dar es salaam katika kikao kilichowashirikisha wafanyakazi wote wa RITA na kuongeza kwamba RITA ni taasisi nyeti sana inayotoa huduma zake mpaka ngazi ya chini ya wananchi hivyo ni lazima kujipanga kikamilifu ili kuweza kuwafikia wananchi wote wanaohitaji huduma na kuondoa malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara.
Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan alimteua Bw. Frank Kanyusi kuwa Kabidhi Wasii Mkuu na Bi. Irene Lesulie kuwa Naibu Kabidhi Wasii Mkuu kuchukua nafasi za watangulizi wao ambao uteuzi wao uliteguliwa.
‘Ili kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi ni lazima tuhakikishe tunaimarisha zaidi atumizi ya TEHAMA ambapo wananchi kutoka maeneo mbalimbali wataweza kupata huduma bila kufika ofisi za Wakala hivyo kupata huduma kwa haraka na kwa gharama nafuu na hili litakuwa moja ya mambo ya msingi tutakayoyasimamia kikamilifu katika uongozi wetu”. Alisema Bw. Kanyusi.

Bw. Kanyusi ameongeza kwamba anafahamu upo mfumo wa RITA ambao wananchi wanautumia kutuma maombi ya huduma hivyo watakaa na wataalamu na kuufanyia tathmini ili kubaini iwapo itahitajika maboresho yanayotakiwa ili uweze kufanya kazi kwa ufanisi zaidi ili ifike wakati maombi yote yawe yanatumwa na kujibiwa kidijitali.
Kwa upande wake Naibu Kabidhi Wasii Mkuu, Bi. Irene Lesulie amewataka watumishi wote kuzifahamu na kuziishi Dira na Dhima za taasisi ambazo zinasimama katika misingi ya kulinda haki na kutoa huduma bora kwa wananchi kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazotuwaongoza.

Pia, amesisitiza kwamba watumishi wote wanatakiwa kutunza siri za Ofisi, kuwa na nidhamu ya hali ya juu, kutumia lugha zenye staha ili kuhakikisha wananchi wote wanaridhika na huduma zinazotolewa na wakala.
‘’Inabidi tuache kufanya kazi kwa mazoea na tuwe wabunifu katika utekelezaji wa majukumu kwani tuko hapa kuwahudumia wananchi na naahidi kwamba tutaendelea kuwatambua na kuwapongeza watumishi wanaofanya kazi kwa bidii na kuvuka malengo, na sisi viongozi wenu kwa paoja tunawaahidi ushirikiano na tutafanya kazi kwa uwazi ili kuleta umoja katika taasisi’’. alisema Bi. Irene.
Akizungumza kwa niaba ya Watumishi, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi tawi la RITA Bw. Adam Nkolabigawa aliwakaribisha viongozi hao katika Taasisi na kuwataka watumishi kupawa ushirikiano na kufanya kazi kwa bidii ili kutimiza malengo hivyo kuwapa viongozi nguvu ya kuwatafutia maslahi bora zaidi.

No comments: