ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 20, 2023

HIFADHI YA AKIBA MKUNGUNERO KUTOA MAFUNZO KWA WANA VIJIJI JINSI YA KUKABILIANA NA TEMBO WANAOVAMIA


HIFADHI ya Pori la Akiba Mkungunero imesema iko kwenye mkakati wa kuanza kutoa mafunzo kwa wana vijiji wanaozunguka pori hilo wilayani Kondoa kama hatua mojawapo ya kuwezesha wananchi kukabiliana na tembo wanaovamia vijiji hivyo na kusababisha uharibifu wa mali pamoja na mazao.

Akizungumza mbele ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Daniel Chongolo ambaye yuko kwenye wilaya hiyo kwa ziara ya kikazi, Ofisa Mhifadhi na Kamanda wa Pori la Hifadhi ya Akiba Mkungunero Floravick Kalambo amesema katika kukabiliana na tembo wavamizi wameweka mipango ya kutoa mafunzo kwa wana vijiji ambao watakuwa sehemu ya kukabiliana na tembo hao.
Akijibu hoja ya tembo kuvamia katika makazi ya vijiji , amesema ni kweli wamekuwa na changamoto na sio tu kwenye pori hilo bali na maneo mengine ya uhifadhi na kwa kuanzia baada ya tembo kuwa wengi Serikali imepeleka fedha na kijiji kilitoa eneo kwa ajili ya kujenga kituo cha kudhibiti wanyama pori wakali na waharibifu.

“Na kutambua umuhimu wa jamii ambayo imetuzunguka sisi pori letu peke yetu hatuwezi kupamabana na hao tembo ambao wametoka vijijini , tunashirikiana na wana vijiji katika kulinda hawa tembo na kwa mara ya kwanza sasa tumechukua mgambo kutoka kwenye vijiji ambao tayari wamepata ajira.

“Na wako kwenye kituo chetu na wanajiandaa kwenda kwenye mafunzo ya namna gani ya kupambana na tembo, lakini kama ambavyo mnaelewa tembo amekuwa mnyama anayebadilika tabia mara kwa mara na sisi tumeliona hilo kwa kushirikiana na watalaam wenzetu kutoka TAWIRI…
“Tunaandaa mkakati wa kuja kufundisha vijiji vyetu vyote ambapo kwa upande wa kondoa na Dodoma kuna vijiji tisa ambavyo tunapambana navyo na watalaam wanajiandaa kuja kufundisha kwenye vijiji na kuja kufundisha wana vijiji kwa ajili ya kupambana na tembo.Niendelee kuwasihi tembo akiwa ametoka eneo la hifadhi msipambane naye kwa kumpiga toeni taarifa kwetu ili tuwarejeshe katika kipindi hiki ambacho bado hamjapata mafunzo.”
Hata hivyo amesema ukiona majirani zao wanalia kwamba tembo wameongezeka hiyo inaamana ya kwamba vijana waliopewa dhamana ya kulinda rasimali za taifa wanafanya kazi vizuri na kile ambacho wametumwa kusimamia kimeanza kuonekana.
“Na mimi naisihi Serikali ya CCM iendelee kutangaza utalii kwasababu wanyama wapo na wanaonekana na ushuhuda huo umeupata kijijini kwetu ambao umeusikia leo kuhusu tembo kuwa wengi.”
Awali wakati anazungumza mbele ya Katibu Mkuu na wananchi, …amesema pori hilo wanamshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuhakikisha utalii unaendelea kwa kasi nchini kwa kuamua kufanya filamu ya Royal Tour ambayo inaweza kwenda kufungua maeneo yao kwa ajili ya utalii.
“Na katika mizunguko yake mingi nipende kumshukuru Rais Samia kwasababu ameweza kutupatia fedha za UVICO-19 ambazo zimetusaidia kujenga barabara za utalii na lango kwa ajili ya kupokelea wageni.

No comments: