ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 6, 2023

RAIS DKT. SAMIA KUFANYA ZIARA YA SIKU NNE NCHINI INDIA

Lengo la ziara ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuendelea kudumisha ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na India hususan sekta za kimkakati kama afya, viwanda na biashara, ulinzi na usalama, elimu, teknolojia ya habari na mawasiliano, uchumi wa buluu, maji, na kilimo.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan atafanya ziara ya Kitaifa nchini India kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya India Mhe. Droupadi Murmu, kuanzia tarehe 8 – 11 Oktoba.

Na Sophia Kingimali

Rais wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan anatarajia kufanya ziara ya kikazi ya siku nne nchini India yenye lengo la kutanua wigo wa biashara na uwekezaji nchini.

Akizungumzia ziara hiyo Oktoba 5 jijini Dar es salaam Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makambo amesema ziara hiyo inatarajiwa kuwa yenye tija kubwa kwa nchi kwani mikataba zaidi ya 15 itasainiwa.

“Ziara hii inafanyika kutokana na uhusiano mzuri uliopo baina ya India na Tanzania lakini pia kudumisha na kuendeleza uhusiano katika sekta za kimkakati ikiwemo elimu,maji,kilimo na afya”amesema Makamba.

Amesema matarajio yanayotegemewa kutokana na ziara hiyo ni pamoja na kuanzisha taasisi ya upandikizaji moyo nchini lakini pia kuanzishwa kwa kiwanda cha chanjo za binadamu na wanyama.

Amesema pamoja na hayo wanatarajia mapinduzi ya kidigitali katika sekta viwanda kwa kuanzisha kiwanda cha kutengenezea simu janja nchini.

Akizungumzia sekta ya kilimo amesema kwenye ziara hiyo inatarajiwa kuja na suluhisho la kudumu la soko la mbaazi nchini India kwani itatoa fursa kwa wakulima kulima zao hilo kibiashara kwani watakua na uhakika wa soko.

“Mbaazi ya Tanzania inaubora sana tutafanya mazungumzo na serikali ya India ili zao hili na mengine yawe na uhakika wa soko India na nchi nyingine.

Sambamba na hayo katika ziara hiyo mawazari wa nchi zote watakutana na kuzungumza namna nzuri ya kushirikiana katika sekta mbalimbali ikiwemo uwanzishwaji wa kongani ya viwanda.

Amesema Rais atapata nafasi ya kukutana na wafanyabiasha wakubwa 15 nchini humo ili kuzungumza nao kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali.

Amesema pia serikali ya India itapata fursa ya kuja kuanzisha karakana ya vyombo vya usafiri wa majini hapa nchini.

Aidha wafanyabiashara 80 kutoka nchini wanatarajiwa kwenda kukutana na wafanyabiashara wa India lakini pia kituo cha uwekezaji TIC na ZIPA nao watashiriki ili kuonyesha fursa za uwekezaji zilizopo nchini.

Rais Dkt Samia Suluhu anatarajiwa kuondoka nchini Oktoba 8 kwa ziara ya siku nne na atawasili nchini India na kupokelewa rasmi kwa ziara ya kitaifa na ataongozana na mawaziri wa wizara mbalimbali ili kuhakikisha sekta ya biashara na uwekezaji inakua nchini.

No comments: