Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Magadula Humphrey Mtafungwa
Binti aitwaye Joyce Hezron (17) Mkazi wa Mtaa wa Magadula kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga, ambaye pia ni Mwanafunzi wa kidato cha tatu Shule ya sekondari Mazinge katika Manispaa ya Shinyanga amefariki dunia kwa kile kinachosadikiwa kuwa amekunywa sumu.
Kwa mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo wameeleza kuwa chanzo cha kifo chake kimetokana na kunywa sumu baada ya kugombezwa na babu yake, akituhumiwa kutumia fedha iliyotumwa kwenye simu yake kwa bahati mbaya.
Wameeleza kuwa kabla ya kifo chake Msichana huyo alipokea muamala wa fedha kiasi cha shilingi elfu sitini,ambayo ilitakiwa kutumwa kwa bibi yake lakini kwa bahati mbaya ikaingia kwake na kwamba aliitumia kwa matumizi binafsi bila idhini ya wakubwa.
Misalaba Media,imezungumza na Mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Magadula Humphrey Mtafungwa ambaye amekiri kuwa na taarifa za kifo cha msichana huyo mkazi wa mtaa wake,ambapo ametumia nafasi hiyo kuwaomba wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao ili kuwaelekeza zaidi kuhusu mambo yanayofaa na yasiyofaa.
“Asubuhi kwenye saa mbili na nusu nilipigiwa simu na balozi akinitaarifu kuwa katika mtaa wangu kuna msiba umetokea usiku wa jana saa nne, nilipofika kwenye eneo la tukio niliongea na familia wakanieleza kweli msiba umetokea na alikuwa ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya Mazinge sekondari mpaka sasa hivi taratibu za maziko zinaendelea tunatarajia kuhifadhi mwili siku ya Jumanne”,amesema Mtafungwa
Chanzo _ Misalaba Media
No comments:
Post a Comment