Wanafunzi waliokamatwa mnadani wakipanda kwenye gari la polisi
NA MWANDISHI WETU
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude kwa kushirikiana na jeshi la polisi wamefika katika mnada wa Mhunze kwa ajili ya Operasheni ya kuwasaka na kuwakusanya wanafunzi ambao hawajafika wala kuripoti shuleni tangu shule zilipofunguliwa Januari 8, 2024.
Msako huo umefanyika leo Alhamisi 11,2024 kufuatia ziara aliyofanya Januari 8 katika shule za sekondari za Isoso na Kishapu na kukuta mahudhurio hafifu.
Katika ziara hiyo alikuta wanafunzi 6 pekee kati ya 138 katika shule ya sekondari Isoso ndiyo wameripoti kuanza masomo ya kidato cha kwanza tangu shule zilipofunguliwa huku katika shule ya sekondari ya Kishapu wanafunzi 56 kati ya 256 waliochaguliwa kuanza masomo ya kidato cha kwanza katika shule hiyo walikuwa wameripoti shule.
Mahudhuri hafifu hayo yamepelekea Mkuu huyo wa Wilaya kuendesha msako kwa wanafunzi ambao hawajaripoti katika maeneo mbalimbali ikiwemo mnadani ambapo amefanikiwa kukusanya jumla ya watoto 45 waliokuwa wakizurura mnadani hapo hali iliyopelekea kuwatafuta wazazi wa watoto hao na kuwataka kuwapelekaa shule watoto hao ili wakaanze masomo yao.
“Haiwezekani serikali imejenga madarasa mazuri na vifaa vyote vya kufundishia vipo walimu wapo halafu wanafunzi hawaripoti shuleni na kuwaachia shule walimu pekee hii haikubaliki”,amesema Mkude
Akizungumzia tukio hilo mkuu wa Dawati la Jinsia wilaya ya Kishapu Inspekta Rose Mbwambo amesema kitendo cha wazazi kutokuwaruhusu watoto wao kuanza masomo nao ni aina ya ukatili kwani elimu ni mojawapo ya haki za watoto wanazotakiwa kuzipata ili kuwa na mustakabali mzuri wa maisha yao ya baadaye katika kutimiza ndoto zao.
Aidha Rose amesema baada ya kuafanya mahojiano na watoto hao baadhi yao wamesema wanakuja mnadani kutafuta mahitaji ya familia ambapo amesema jukumu hilo si la mtoto bali ni la mzazi.
“Niwaambie tu wazazi wa watoto ambao wamekutwa mnadani na ambao wako majumbani watoto wote wanaotakiwa kuwa shule , watambue ni kosa kisheria kumkosesha elimu mtoto”amesema rose
Nao baadhi ya wazazi waliofika katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Kishapu baada ya watoto wao kuchukuliwa katika mnada huo wamesema sababu kubwa inayochangia watoto hao kutoripoti shuleni kwa ajili ya kuanza masomo ni uchumi,kwani hawajapata fedha za kununua mahitaji yanayotakiwa shuleni.
‘’Kinachosumbua mheshimiwa mkuu wa wilaya ni uchumi , hatuna fedha ya mahitaji kwa ajili ya kununua vifaa vinavyohitajika shule, fedha haijapatikana lakini tunajitahidi Jumatatu tutawapeleka watoto shuleni”,amesema masemwa Tambilija kwa niaba ya wazazi wa watoto hao.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude akiwahoji wanafunzi waliokutwa mnadani
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude akiwahoji wanafunzi waliokutwa mnadani
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude akiwahoji wanafunzi waliokutwa mnadani
No comments:
Post a Comment