Thursday, February 8, 2024

HIZI NDIZO ALAMA ALIZOACHA OLE MUSHI



Maziko ya mchambuzi na mchangiaji wa mijadala kwenye mitandao ya kijamii, Thadei Mushi maarufu Thadei Ole Mushi yamewakutanisha viongozi wa kisiasa kutoka vyama mbalimbali mkoani Kilimanjaro, wakitaja alama alizoacha zikiwamo ushupavu na kusimamia ukweli bila woga.

Ole Mushi aliyefariki dunia Februari 4, 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alikokuwa akipatiwa matibabu ya matatizo ya moyo, amezikwa leo Februari 7, 2024 nyumbani kwao kijijini Shinga, wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.

Katika maziko ya Ole Mushi ambaye kitaalumu alikuwa mwalimu, mamia ya waombolezaji walihudhuria akiwemo Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete.

Viongozi wa kisiasa waliopata fursa ya kuzungumza, wamemwelezea Ole Mushi, kama kijana aliyekuwa jasiri, mwenye msimamo na aliyeweza kukosoa mambo aliyoona yanakwenda kinyume bila woga.

Miongoni mwa wanasiasa hao ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, Mwenyekiti wa Chadema mkoani hapa, Michael Kilawila, Makamu mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Taifa, Joseph Selasini na baadhi ya wakuu wa wilaya za mkoa huu.

Boisafi akimzungumzia Ole Mushi aliyekuwa kada wa CCM, amesema chama hicho kitatafuta nyaraka mbalimbali alizoandika enzi za uhai wake ili kuweka kumbukumbu na kuzitumia kukiwezesha kusonga mbele.

"Thadei alikuwa ni mwalimu kwetu, kupitia salamu tulizozipata kwa wengi, kuna mambo ambayo tumejifunza na haya ndiyo tunayotakiwa kutoka nayo hapa, kwamba unapopata nafasi kwa umri ambao utakuwa nao, kwenye kufanya jambo lolote, kwanza jiamini, jitosheleze halafu useme, na huyu ndiye aliyekuwa Thadei Ole Mushi," amesema.

Amesema, "Ole Mushi alikuwa hasemi bila kufanya utafiti na hasemi kwa malengo ya kumuonea mtu, alikuwa anasema kwa sababu alikuwa anaamini anachosema, tunajua kama mwanachama wa CCM, tumepoteza kada mwaminifu, mweledi, mchambuzi wa mambo mengi ya kisiasa na alisimama imara."

"Tualike vijana wengine mwenye umri au chini yake au katikati yake, wawe watu wa kusema ukweli, CCM ndivyo tulivyo, alikuwa ni mpatanishi na CCM tunayo tuliyojifunza kwake, hayo tutayaishi," amesema.

Amesema CCM itatafuta nyaraka alizoziandika Ole Mushi na kuziweke kwenye kumbukumbu ili yale yanayokisukuma chama hicho mbele, watayaweka kuhakikisha hakuna kinachopotea.

Kwa upande wake, Kilawila amesema Taifa limepoteza kiungo mwadilifu, ambaye alikuwa msuluhishi wakati walipotofautiana kutokana na itikadi za kisiasa kwenye majukwa ya kisiasa.

"Taifa limepoteza kiungo mwadilifu ambaye hata pale tulipohitilafiana kulingana na itikadi zetu za vyama vyetu, yeye ndiye aliyekuwa msuluhishi na kutujenga, ni kijana mdogo lakini alikuwa na karama ya kutuweka pamoja hadi siku anafariki dunia," amesema na kuongeza:

"Kwa sababu kisima kile ambacho tulikuwa tunachota busara sasa kimekauka, naamini kati yetu sisi atazaliwa Thadei ambaye ataunganisha Mkoa wa Kilimanjaro ili tuweze kuimba wimbo mmoja wa maendeleo ya mkoa huu na Tanzania tunayoitaka kesho. Hakusita kukosoa kutoka mahali popote pale ambapo aliona panaenda ndivyo sivyo, tuendelee kupendana na kuipigania Kilimanjaro yetu."

Selasini amesema Ole Mushi alipendwa na kila mtu kwa sababu ya bidii yake katika kazi na alisimama kutekeleza majukumu yake akitetea haki za wengine bila kujali itikadi yake ya kisiasa.

"Wengi tunamlilia Thadei kwa sababu ya bidii yake katika kazi, alikuwa akitekeleza majukumu yake akitetea haki za wote na hakujionyesha kwamba anamilikiwa na CCM peke yake, alikuwa ni wa vyama vyote na alitushauri sote lakini hakukiacha chama chake," amesema.

"Poleni CCM kwa kumpoteza kada muhimu, naomba vijana wa Kilimanjaro mjengwe katika tabia ya Thadei, popote mtakapokuwa iwe CCM, Chadema, NCCR, mjengwe na tabia ya utaifa aliyoonyesha Mushi," amesema.

Ridhiwani akitoa salamu kwa niaba ya Serikali, amesema Ole Mushi hakuwa mtu wa kutaka vyeo, na mara zote alisimamia ukweli kwenye kueleza jambo penye uongo alisimama kuweka sawa.

"Thadei hakuwa mwoga na ukitafakari maisha yake ndiyo maisha ya mwana-CCM wa kweli, huyu hakuwa wale wataka vyeo, penye ukweli alinyooka, penye uongo anaweka sawa, hicho ndicho Chama cha Mapinduzi na ndivyo tulivyoishi wengine," amesema.



No comments: