Na Mwandishi wetu.
Imeelezwa kuwa upatikanaji miundombinu ya maji safi iliyounganishwa na miundombinu ya umeme katika vijiji vya Nyanguge na Bunamhala Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu imekuwa mwarobaini katika kupambana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu.
Hii ni baada ya Wizara ya Afya,kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) katika kutekeleza mradi wa kupambana na Magonjwa ya Mlipuko ikiwemo Kipindupindu na Uviko-19 kusambaza umeme katika visima ambavyo havikuwa na pampu za umeme za kuvuta maji.
Wakizungumza baadhi ya wananchi walionufaika na mradi huo kutoka vijiji vya Nyanguge na Bunamhala Wilayani Bariadi Mkoani Simiyu wamesema kipindi cha nyuma walikuwa wanachota maji kutoka vyanzo mbalimbali visivyosalama ikiwemo kwenye madimbwi hali iliyopelekea kuwa na changamoto ya magonjwa ya mlipuko ikiwemo kuhara na kutapika ila kwa sasa hali ni shwari.
“Kipindi cha nyuma kulikuwa na changamoto mbalimbali za mlipuko wa magonjwa kutokana na kuchota maji mlimani na kwenye madimbwi lakini baada ya huu mradi umetusaidia sana magonjwa yamepungua ikiwemo Kipindupindu “amesema John Nshashi.
Bashiri Salum ni Afisa Afya na Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma Mkoani Simiyu amesema katika kuhakikisha maji yanakuwa safi na salama kwa afya ya binadamu huwa yanawekewa dawa ya Klorini ambapo yamekuwa yakitumika kwa matumizi mbalimbali .
“dawa ya klorini huwa inatuhakikishia usalama ,na maji haya yamekuwa na msaada mkubwa kama tunavyofahamu magonjwa ya mlipuko huwa yanatoka kwa kuzingatia kanuni za afya ikiwemo kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni hivyo uwepo wa maji haya umesaidia na kutuhakikishia kuna maji safi na salama”amesema Bashiri.
Mradi wa wa kupambana na Magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu na UVIKO-19 unatekelezwa katika Wilaya za Bariadi, Itilima, Busega na Maswa katika Mkoa wa Simiyu na ukitekelezwa kwa mikoa mitano kanda ya ziwa ambayo ni Simiyu, Mwanza, Mara, Kagera na Geita lengo likiwa ni upatikanaji wa umeme vijjini kurahisisha upatikanaji wa maji safi na salama katika jamii ambapo huduma hiyo imeunganishwa pia katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya.
No comments:
Post a Comment