Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema Serikali imeamua kutekeleza miradi mipya ya uzalishaji wa umeme badala ya kutegemea vyanzo vya zamani ili kuendana na ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme nchini.
Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 08 Februari, 2024 Jijini Dodoma baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 49.5 kwa nguvu ya maji katika Mto Malagarasi mkoani Kigoma. Mkataba huo umesainiwa na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) na kampuni ya Dongfang Electric International kutoka Jamhuri ya Watu wa China.
“Lazima tuwe na vyanzo vingi na vipya vya umeme, kiu na njaa ya umeme tuliyonayo inatufanya tufikirie namna ya kupata umeme kwa haraka, mahitaji ya umeme yameongezeka sana lakini vyanzo ni vilevile kwa miaka mingi mfano Bwawa la Mtera lilijengwa mwaka 1980, Kidatu mwaka 1975, Kihansi mwaka 2000, Pangani 1995, Hale 1968, Nyumba ya Mungu 1964 na mwaka 2019 baada ya Gesi kuanza uzalishaji umeme mahitaji yalikuwa pungufu kuliko uzalishaji, lakini sasa mahitaji ni makubwa kuliko vyanzo.” Amesema Dkt. Biteko
Amesema kutokana na mahitaji ya umeme kuwa makubwa kuliko vyanzo vyake, Serikali inaendelea kuongeza vyanzo vipya ikiwemo mradi wa Malagarasi ambao utekelezaji wake utachukua miezi 42 na utekelezaji wa mradi wa Julius Nyerere (JNHPP) ambao kwa sasa umekamilika kwa asilimia 96 na unatarajia kuingiza umeme kwenye gridi ya Taifa mwezi huu.
Ili kuwa na umeme kutoka vyanzo mchanganyiko, Dkt, Biteko ametanabaisha kuwa, ameshatoa maagizo kwa watendaji wa Wizara na TANESCO kuhakikisha wanabadilika na kuboresha huduma zao kwa wananchi na kuwezesha uwekezaji katika miradi ya kuzalisha umeme kwa nguvu ya Jua na Upepo.
Akizungumzia hali ya umeme Mkoani Kigoma, Dkt. Biteko amesema Pamoja na mradi wa Mto Malagarasi, kuna miradi mingine mitatu ikiwemo usafirishaji wa umeme kutoka Nyakanazi hadi Kigoma (kV 400), Tabora hadi Kigoma (kV 132), kuongezwa uwezo wa kituo cha umeme wa Jua cha Kigoma kutoka megawati 5 hadi megawati 10.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa uboreshaji wa miundombinu nchi nzima unaendelea na hii inajumuisha ujenzi wa vituo vya kupoza umeme katika maeneo mbalimbali nchini na kwa kuanzia vinajengwa vituo 24 katika maeneo ya kimkakati ili kutengemaza gridi ya Taifa.
Aidha, ameishukuru Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa kutoa mkopo wa masharti nafuu wa kiasi cha Dola za Marekani milioni 140 ili kutekeleza mradi wa Malagarasi ambapo Serikali ya Tanzania imetoa Dola za Marekani Milioni 4.14. Amesema Benki hiyo imeendelea kuiunga mkono Serikali katika miradi mbalimbali nchini.
Vilevile, amewaagiza Wakandarasi kutekeleza mradi huo kwa haraka na ufanisi kama ilivyo kwa mradi wa umeme wa JNHPP ili wananchi wa Kigoma na nchi nzima wapate umeme wa uhakika.
Mradi wa Malagarasi unahusisha ujenzi wa eneo la kufua umeme wa maji, njia za kupitisha maji, jumba la mitambo ya umeme, kituo cha kupokea na kusafirisha umeme, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 132 ambayo itaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa kupitia kituo cha Kidahwe- Kigoma na kuunganisha umeme kwenye vijiji 7 vitakavyopitiwa na mradi.
Akizungumza kabla ya utiaji Saini, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhe. Profesa Joyce Ndalichako amesema mbali na uzalishaji wa megawati 49.5 kuongeza kiwango cha umeme katika gridi ya Taifa, pia hatua hiyo itachochea uanzishaji na ukuaji wa viwanda katika mkoa wa Kigoma.
Ameongeza kuwa kupitia hali hiyo, ajira zitaongezeka na kuwezesha wananchi kushiriki katika kukuza Uchumi wa Mkoa wa Kigoma na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amesema maono na maelekezo ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu uzalishaji wa nishati mkoani humo yameuheshimisha Mkoa wa Kigoma na Taifa kwa ujumla.
Amesema uzalishaji wa megawati 49.5 za umeme utapunguza gharama za uendeshaji ambapo kwa sasa zinatumika lita 28,000 za mafuta kwa siku kwa ajili ya kuzalisha umeme.
Viongozi wengine walioshuhudia utiaji Saini ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, Wabunge kutoka Mkoa wa Kigoma, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Kilumbe Ng’enda.
No comments:
Post a Comment