ANGALIA LIVE NEWS

Monday, February 5, 2024

WAZIRI JAFO-BIASHARA YA KABONI KUINGIZIA PATO LA TAIFA


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema Serikali inatarajia kupata wastani wa shilingi trilioni 2.4 kutokana na biashara ya kaboni ambazo zitachangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la Taifa.

Dkt. Jafo ameliarifu Bunge leo Februari 5, 2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Buhigwe Mhe. Kavejuru Felix aliyetaka kujua biashara ya kaboni katika misitu ya asili na ya kupanda imechangia kiasi gani kwenye pato la taifa tangu iingie nchini.

Wamesema hadi kufikia Desemba 31, 2023 Serikali imepokea jumla ya maombi 35 ya miradi mbalimbali ya biashara hiyo pindi mchakato wa usajili utakapokamilika na kuanza kutekelezwa kwa miradi hii.

“Katika miaka ya hivi karibuni kumeibuka soko huria la biashara ya kaboni ikijumuisha misitu ya asili na ya kupanda na imeanza kushamiri hapa nchini na kuonesha inaweza kuchangia kwenye pato la taifa,” alisema Dkt. Jafo.

Halikadhalika, Waziri Jafo alisema katika kipindi cha mwaka 2018-22 fedha zilizopokelewa kupitia miradi inayotekelezwa kwenye halmashauri mbalimbali hapa nchini inafikia shilingi bilioni 32.

Akiendelea kujibu maswali ya nyongeza kuhusu mkakati wa utoaji elimu ya biashara hiyo, Dkt. Jafo alisema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEM pamoja na Wizara ya Maliasili na Utali imefanya mkutano na wakuu wa mikoa na wilaya kupeleka ujumbe.

Aliongeza kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kutoa elimu kwa wananchi na kuwahamasisha kupanda miti kwa wingi ili kunufaika na biashara hiyo na kuhifadhi mazingira.

Pamoja na hayo, Waziri Jafo alisema pia Tanzania imetumia fursa ya ushiriki katika Mkutano wa 28 Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika Dubai, Falme za Kiarabu kutangaza biashara ya kaboni.

Kutokana na hatua hiyo alisema kuwa mwitikio wa wananchi na kampuni za ndani na nje kushiriki katika biashara ya kaboni umekuwa mkubwa hivyo kuongeza pato la taifa.

No comments: