Chuo cha Usafiri wa Anga nchini (CATC) kinaendesha mafunzo ya Usalama wa Usafiri wa anga kwa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) yakilenga kutambua na kudhibiti vihatarishi mbalimbali vinavyoweza kujitokeza katika viwanja vya ndege vinavyoendeshwa na shirika hilo.
Akieleza juu ya mafunzo hayo ya siku 5 kuanzia Machi 04, 2024 -Machi 08, 2024 yanayofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi mkoani Morogoro , Mkufunzi Mkuu wa CATC Thamarat Abeid alisema lengo la mafunzo hayo ni kutoa elimu inayohusiana na usalama katika viwanja vya ndege kwa kutumia sheria, kanuni na taratibu za Shirika la Usafiri wa Anga duniani - ( ICAO), pamoja na kanuni na taratibu ambazo zimetolewa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ili wataalam wafanye kazi kwa ufasaha na kuleta tija kwa taifa na dunia kwa ujumla.
Aidha, mkufunzi huyo aliongeza kuwa mafunzo haya yanahusisha vihatarishi mbalimbali vilivyopo katika viwanja vya ndege, utoaji wa taarifa ambazo ni muhimu sana ili wamiliki wa ndege na marubani wapate wigo mpana wa uelewa hata kama itatokea changamoto ijadiliwe kwa pamoja na kupata mwafaka wa pamoja kati ya wamiliki wa viwanja, marubani, wamiliki wa ndege na Mamlaka ya Usafiri wa Anga.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa TANAPA Fredrick I. Malisa akimwakilisha kamanda wa Kanda ya Mashariki, amewashukuru wakufunzi wa mafunzo hayo na kuwadokeza kuwa usafiri wa anga kwa upande wa TANAPA ni nguzo muhimu sana katika mnyororo wa kukuza utalii nchini.
Na kuongeza kuwa kwa kutambua umuhimu huo katika kipindi cha takribani miaka minne Serikali imewekeza zaidi ya Shilingi Bilioni 130 katika maboresho ya viwanja vya ndege vinavyoendeshwa na TANAPA pamoja na manunuzi ya mitambo na vifaa vya ujenzi ili kuendana na kasi ya utalii na usalama wa watalii na hatimaye kuweza kufikia malengo ya kitaifa ya idadi ya watalii Milioni tano na Mapato Shilingi Bilioni sita ifikapo mwaka 2025/2026.
Aidha, Kamishna msaidizi wa uhifadhi Fredrick I. Malisa alisema, TANAPA inatambua umuhimu wa kazi za usalama wa viwanja vya ndege kufanyika kwa ufanisi, hivyo ni lazima watumishi wanaofanya kazi hizo kujengewa uwezo, na ndio msingi wa mafunzo hayo ya kibobezi yanayotolewa na wakufunzi wa CATC .
Hafla ya ufunguzi wa mafunzo hayo ilihudhuriwa pia na Afisa Uhifadhi Mkuu anayesimamia viwanja vya ndege TANAPA, Christine Bgoya pamoja na mkuu wa Hifadhi ya Taifa Mikumi kamishna msaidizi wa uhifadhi Augustine Masesa
Mafunzo hayo kwa TANAPA yamehusisha maafisa na Askari kutoka Idara ya Miundombinu na wengine ambao wanahusika moja kwa moja na masuala haya ya utekelezaji wa kanuni za usalama wa viwanja vyetu vya ndege kutoka hifadhi 11 na TANAPA makao makuu.
No comments:
Post a Comment