ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 4, 2024

KAMATI YA USALAMA BARABARANI YAKABIDHI MAGARI NA PIKIPIKI KWA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA


KAMATI ya Usalama barabarani Mkoa wa Mbeya imekabidhi magari mawili na pikipiki mbili kwa Jeshi la Polisi ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu hasa doria za barabara kuu, utoaji wa elimu na kudhibiti ukiukwaji wa sheria za usalama.
Akizungumza na waandishi wa habari Machi 04, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Benjamin Kuzaga katika hafla fupi ya mapokezi ya magari na Pikipiki ameishukuru Kamati ya Usalama barabarani Mkoa wa Mbeya kwa msaada wa magari na Pikipiki hizo kwani zitasaidia sana katika kufanikisha kutekeleza majukumu kwa ufanisi na haraka.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama barabarani Mkoa wa Mbeya Mhandisi Rajabu Ghuliku ameeleza kuwa "Kamati imeona vema kutoa msaada wa pikipiki na magari kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu katika Kikosi cha Usalama barabarani Mkoani Mbeya"

Aidha, Mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Mbeya Mrakibu wa Polisi Hussein Gawile amesema kuwa, vitendea kazi hivyo vinakwenda kuongeza ufanisi na nguvu katika kuzuia na kudhibiti ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.

Jumla ya magari mawili na pikipiki mbili yenye thamani zaidi shilingi Milioni 31 yamekabidhiwa katika hafla hiyo.

No comments: