Advertisements

Tuesday, April 23, 2024

ZANZIBAR YAUNGANA NA DUNIA KUADHIMISHA KILELE CHA WIKI YA MAABARA DUNIANI


Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui akikata utepe kuashiria uzinduzi wa sera ya maabara Zanzibar katika kilele cha wiki ya maabara iliyofanyika ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa ndege Zanzibar.

Na Fauzia Mussa, Maelezo
Raisi wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka wataalamu wa Maabara kuvifanyia utafiti vitu wanavyovichunguza ikiwemo maradhi ili kuyadhibiti kwa njia za kisayansi.

Akisoma hotuba ya Rais Mwinyi katika kilele cha wiki ya Maabara Duniani huko Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege Zanzibar alipomwakilisha, Waziri wa Afya Zanzibar Nassor Ahmed Mazrui amesema kufanya hivyo kutasaidia taasisi kudhibiti maradhi na kuzielekeza njia zinazoshauriwa kirahisi kutokana na kuwepo na ushahidi wa Kisayansi.

Aidha amewataka wataalamu hao kuongeza nguvu kwenye Taasisi za Tafiti ikiwemo za Taaisi ya Afya ya Binaadamu (ZAHRI), Utafiti wa Mifugo (ZALIRI), Taasisi ya Utafiti wa Safayansi ya Baharini (ZAFIRI) ili kuweza kufikia malengo yaliokusudiwa.

Amefahamisha kuwa Maabara zote zina mchango mkubwa kwa maendeleo mbalimbali ikiwemo ya afya na huduma zinazotolewa kwa wananchi, hivyo Serikali itaendelea kuimarisha Maabara zote ili kuweza kuendeleza kazi za uchunguzi wa maradhi, vinasaba, kemikali, pamoja na vyakula.

Akizungumzia Sera ya Maabara Zanzibar, amesema ni jambo zuri kwani utekelezaji wa kazi za vipimo hasa zinapokuwa zinatekelezwa na wadau tofauti ni vyema kuwepo na Miongozo itakayosaidia kulinda mipaka ya kiutendaji, ubora na viwango vinavyojali maslahi mapana ya wanaotegemea huduma kwenye Taasisi hizo.

Aidha amewasisitiza kushirikiana na kufanya kazi na Viongozi pamoja na mashirika ya kimataifa yanayoshughulikia maendeleo kwa lengo la kuleta maendeleo ya kweli kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Hata hivyo, amewatakaWataalamu hao kufanya mapitio ya mipango kazi yao kila robo ya mwaka ,miezi sinta na mwaka ili kuweza kujifanyia tathmini ya mafanikio na kuzitafutia ufumbuzi wa haraka changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Tusisubiri mpaka wiki ya maadhimisho ya maabara ndio mukaanza kufanya kazi hivyo hatuawaza kufikia malengo wa kupata maendeleo ya kweli kama tunavyojua Serikali inatuamini na inatutegemea kupata mambo mazur kutoka kwetu.” alisema Kiongozi huyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya Dkt. Amour Suleiman amesema lengo la maadhimisho ya wataalamu wa maabara Zanzibar ni kuungana na wataalamu wengine Duniani na kuona umuhimu wa kazi za Ki –Maabara katika kutoa huduma kwa jamii.

Alifahamisha kuwa Dunia huadhimisha siku hiyo kwa Wataalamu wa Maabara za Afya pekee, lakini kwa upande wa Zanzibar sekta tofautizimeshiriki kuadhimisha wiki hiyo ikiwemo maabara za Afya, Kilimo, Mifugo, Maji (ZAWA), ZBS , ZFDA ,MKEMIA MKUU na ZURA ili kuweka nadharia ya Afya mjumuisho.

Wakitoa salamu za wadau wa maendeleo Mkururugenzi mkaazi wa shirika la ICAP Nchini Tanzania Haruka Maruyama na Wangeci Gatei wa CDC Tanzanzia wamesema kupitia Maabara zilizojengwa na kuwa na miumdombinu imara Zanzibar sasa inaweza kujiamini na kuwa na uhakika wa kukabiliana na tishio lolote la miripuko na kulinda afya za wazanzibar wakati yanapotokezea.

Aidha wameahidi kuendelea kufanya kazi na Serikali kupitia Wizara ya Afya ambapo Wizara hiyo imeandaa muongozo wa uwendeshaji wa ufuatiliaji wa maabara, utakaoweza kuimarisha na kugundua mapema magonjwa.

Nao Wataalamu wa maabara wamesema mbali na mafanikio hayo yanayoonekana katika sekta hiyo bado Wataalamu wa Maabara wa Zanzibar hawajaweza kuitumia ipasavyo fursa iliyotangazwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuingia ubia wa uendeshaji wa Maabara za hospitali zilizopo nchini.

“Bado Uendeshaji wa Maabara hizo sio rafiki kwa Wahudumu ambao tayari wapo kwenye mfumo rasmi wa ajira wa Serikali au wanaotegemewa kuingia kwenye mfumo wa Serikali na wabia waliomo kwenye uendeshaji wa Maabara hizo kwa sasa bado hawajatambua kikamilifu umuhimu wa kutumia Wataalamu wa Maabara wa ngazi ya katikati na ile ya wabobezi.” Walisema

Amefahamisha kuwa kada hiyo inakabiliwa na ukosefu wa Waatalamu wahandisi wa vifaa tiba wa kukarabati na kuzifanyia matengenezo ya tahadhari Mashine hizo pale zinapoharibika na kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi na kusabaisha hasara kwani zinanunuliwa kwagharama kubwa.

Aidha Ukosefu wa waatalamu wa Maabara katika Skuli za Sekondary (Laboratory Technicians) kunapelekea kukosekana kwa usimamizi mzuri wa Maabara na kupelekea baadhi ya vifaa kuharibika kwa haraka.

Awali walimshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi juu ya mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta za maabara katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake ambapo huduma za uchunguzi zimeimarika , pamoja na kupatikana kwa ajira za Wataalamu wa kada hiyo na kada nyengine za Afya.

Wamebainisha kuwa Maabara za kisasa zimejengwa katika hospitali zote 11 za wilaya Unguja na Pemba pamoja na ZFDA kufungwa mashine za kisasa ikiwemo ya HPLC.

Wiki ya maabara huadhimishwa kuanzia April 14 hadi 21 dunia kote ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema maabara ni kila kitu.

No comments: