Advertisements

Wednesday, May 22, 2024

ELIMU YA FEDHA YAFIKA MKOA WA KAGERA



Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Erasto Sima, akipokea vipeperushi vilivyo na taarifa mbalimbali za elimu ya fedha ikiwemo uwekaji akiba, uwekezaji, kupanga kwa ajili ya uzeeni, usimamizi binafsi wa fedha na mikopo kutoka kwa Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, baada ya kumalizika kwa kikao kilichofanyika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Bukoba.


Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mhe. Erasto Sima, akizungumza wakati wa kikao na Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha (hawapo pichani) iliyofika ofisini kwake kujitambulisha kwa ajili ya zoezi la utoaji elimu katika Wilaya ya Bukoba, Muleba, Misenyi na Biharamulo mkoani Kagera.

Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, akitaja wilaya Wilaya zitakazofikiwa wakati wa zoezi la kutoa elimu ya fedha Mkoani Kagera, ikiwa ni pamoja na Wilaya ya Bukoba, Muleba, Misenyi na Biharamulo, wakati walipomtembelea ofisini kwa Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Mhe. Erasto Sima (hayupo pichani).

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Erasto Sima akiwa katika kikao na Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha (kulia) na Afisa Biashara Mkoa wa Kagera na Mratibu wa Huduma za Fedha ngazi ya Mkoa, Bw. Keneth Mlilo, kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo mkoani Kagera.

Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Erasto Sima, (wa pili kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Fedha baada ya kumalizika kwa kikao kati yake na Timu hiyo ambapo walijadili namna bora ya kuwafikia wananchi katika zoezi la utoaji elimu. Kutoka kulia ni Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, kushoto ni Afisa Mwandamizi masuala ya Fedha Mamlaka ya Masoko na Mitaji na Dhamana (CMSA) Bi. Gladness Mollel na Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha Bi. Mary Mihigo.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha)


Na. Josephine Majula, WF, Kagera
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Mhe. Erasto Sima, amewataka watoa huduma za Fedha kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa na Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania wakati wa kutoa huduma za fedha kwa wananchi.

Agizo hilo amelitoa alipokutana na Timu ya wataalamu ya Wizara ya Fedha ambao wamefika mkoani Kagera kwa ajili ya kutoa elimu ya huduma za fedha kwa wananchi katika makundi mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, wajasiriamali na wanafunzi.

“Watoa huduma ya fedha msifanye biashara kwa mazoea mfuate utaratibu uliowekwa na Serikali ukiwemo wa kupata leseni kwa mamlaka zinazotambulika kisheria kwa ajili ya kutoa huduma za fedha.”, alisema Mhe. Sima.

Kwa upande wake Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, alisema kuwa kutokana na wananchi wengi kutapeliwa wanapohitaji huduma za fedha, Wizara ya Fedha imeamua kutatua changamoto hiyo kwa kutoa elimu ya fedha kwa njia mbalimbali ikiwemo ya filamu.

Bw. Kibakaya alisema kuwa Timu ya wataalamu itatoa mafunzo hayo kupitia filamu iliyoandaliwa mahususi ikiwa na mada mbalimbali za elimu ya fedha ikiwemo uwekaji akiba, uwekezaji, kuweka mipango kwa ajili ya uzeeni, usimamizi binafsi wa fedha na mikopo.

Naye Mfanyabiashara Bi. Lilian Lugakingira aliishukuru Wizara ya Fedha kwa kuwafikia na kuwapa elimu hiyo muhimu kwa kuwa itawasaidia kuwa na uelewa mpana wa masuala ya fedha.

“Nimefurahi sana kupata elimu ya fedha, nimepata elimu nzuri ya namna bora ya kuweka akiba na kufanya uwekezaji kupitia faida nitakayoipata kwenye biashara yangu, nitawaelimisha wenzangu ili waweze pia kujiwekea akiba na kuwekeza katika Taasisi rasmi ili waweze kupata faida” alisema Bi. Lugakingira.

Katika kutoa elimu kwa wananchi kwenye mikoa hiyo Timu ya wataalamu wa Wizara ya Fedha imeambata na wataalamu kutoka Taasisi nyingine za Serikali ikiwemo Mamlaka ya Masoko na Mitaji na Dhamana (CMSA) na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Wizara ya Fedha imeanza kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa makundi mbalimbali katika mikoa nane ikiwemo Kagera, Singida, Manyara ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa mwaka 2021/2022 hadi 2029/2030.

No comments: