Advertisements

Wednesday, May 8, 2024

FEDHA ZA MFUKO WA JIMBO ZIMEENDELEA KULETA TIJA NA MATOKEO CHANYA KATIKA KUIMARISHA NA KUKUZA UCHUMI


Fedha za Mfuko wa Jimbo zimeendelea kuleta tija na matokeo chanya katika kuimarisha na kukuza uchumi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla na hivyo kuleta manufaa kwa wananchi wa pande zote mbili za Muungano.

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Wingwi Mhe. Omar Issa Kombo kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingir) Mhe. Dkt. Selemani Jafo bungeni.

Katika swali lake Mhe. Kombo alitaka kujua lini Serikali itafanyia kazi changamoto ya Kodi na Tozo kwenye Fedha za Mfuko wa Jimbo kwa upande wa Zanzibar, Naibu Waziri Katambi amesema kuwa kodi na tozo hutozwa kwa mujibu wa Sheria pindi bidhaa au huduma zinapotolewa au kununuliwa.

Aidha, amebainisha kuwa bidhaa na huduma zinazotolewa hukatwa kodi ya zuio la kodi (With Holding Tax) kwa kuzingatia Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura ya 332 chini ya kifungu cha 83 (1) (c) kwa malipo ya ada ya kwa huduma kwa ajili ya utoaji wa huduma ya kitaalamu na kifungu (83 A) malipo kwa bidhaa zinazotolewa na mkazi wa uendeshaji biashara.

Naibu Waziri Katambi amesema kuwa kodi hutozwa kwa kuzingatia Sheria ya Manunuzi inayotumika Zanzibar inayojulikana kama sheria zinazotolewa na mkazi wakati wa undeleshaji biashara.

Serikali imesema imebuni miradi mbalimbali ya kimazingira inayosaidia jamii kuweza kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika maeneo mbalimbali nchini.

Pamoja na hatua hizo pia, imeendelea kuihimiza jamii kutumia nishati mbadala na majiko banifu ili kupungunguza kasi ya ukataji wa misitu ambayo husababisha uharibifu wa mazingira.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Patrobas Katambi wakati akijibu maswali bungeni kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo bungeni jijini Dodoma leo tarehe 06, 2024.

Akijibu swali la Mbunge wa Mwera Mhe. Zahor Mohammed Haji aliyetaka kujua mpango wa Serikali kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika kuwakinga wananchi na madhara yanayoweza kutokea, Mhe. Katambi amesema Serikali inatekeleza miradi ya upandaji miti, usambazaji wa maji safi kwa matumizi ya majumbani na mifugo na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.

Ametaja ujenzi wa kuta katika maeneo ya fukwe za bahari yanayokabiliwa na mmomonyoko wa ardhi, ujenzi matuta na mabwawa kudhibiti mafuriko, kuwezesha jamii kubuni miradi mbadala ya kuongeza kipato na iliyo rafiki kwa mazingira pamoja na urejeshaji wa maeneo ya ardhi yaliyoharibika kuwa ni jitihada zingine za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Akiendelea kujibu swali hilo, Mhe. Katambi amesema Serikali imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (2021), Mpango Kabambe wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032) na Mchango wa Taifa katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (2021) ambayo ina mchango katika kukabiliana na changamoto hiyo.

Ameongeza kuwa Serikali inashirikiana kikamilifu na jumuiya ya kimataifa katika kubuni mikakati na hatua madhubuti za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika ngazi zote ikiwemo kuridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa Kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, Itifaki ya Kyoto na Makubaliano ya Paris.

Aidha, Naibu Waziri Katambi amesema Serikali inaendelea kuelimisha wananchi kuhusu madhara yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi ili waweze kuchukua tahadhari na kujilinda na maafa yanayosababishwa na changamoto hizo, ambapo uelimishaji hufanyika kabla ya maafa kutokea.

No comments: