Friday, July 26, 2024

SPIKA TULIA AMUAPISHA MBUNGE BALOZI KOMBO DAR



Na Andrew Chale, Dar es Salaam.
SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Tulia Ackson amemuapisha Balozi Mahmoud Thabit Kombo kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ofisi ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam.

Balozi Kombo ameapishwa leo Alhamisi Julai 25, 2024, Ofisi hizo huku akiambatana na familia yake, sambamba na kusindikizwa na Wabunge kadhaa pamoja na maafisa wa Bunge n wale wa ofisi ya Mambo ya Nje tukio lililoshuhudiwa na Waandishi wa Habari mbalimbali.

Julai 21, 2024 Balozi Kombo alipoteuliwa kuwa Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Rais Samia Suluhu Hassan, kuchukua nafasi ya January Makamba ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.

Katika tukio hilo, Dk Tulia amempongeza kwa kuaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kupewa nafasi ya ubunge, huku akisema zipo chache hivyo yeye kuwa miongoni mwao ni heshima kubwa.

"Tukio hili ambalo tumelikamilisha hapa ni kiapo cha uaminifu ambacho kinamfanya Balozi Kombo kuwa mbunge kwa matakwa ya ibara ya 68 ya Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na kwa mujibu wa kanuni za Bunge za kudumu.

"Kanuni ya 30 fasili ya kwanza ambayo inaeleza kabla ya mbunge kuanza kushiriki kanuni za Bunge lazima ale kiapo cha uaminifu mbele ya Spika,” amesema Dk Tulia.

Amesema fasili ndogo ya 2(b) inaleza mbunge ataapishwa na Spika kwa mujibu wa eneo ambalo litapangwa na Spika huku akisema awali kulikuwa na changamoto jambo ambalo lilifanya kanuni zibadilishwe.

“Tulilazimika kutoa ufafanuzi huu kila wakati ili watu wasione kwa nini wabunge wengine wanaapishwa bungeni wengine nje ya Bunge, kanuni zetu zinaruhusu hayo mazingira na Spika akiagiza wapi kiapo kitafanyika hapo, leo tumefanyia ofisi ndogo za Bunge hapa Dar es Salaam lakini ingeweza kufanyika sehemu nyingine yoyote,” amesema Dk Tulia.

Dk Tulia amesema anaamini Balozi Kombo na wengine walioteuliwa watakwenda kufanya kazi na kuendeleza mipango ambayo imewekwa wazi na Rais ikiwemo uhusiano wa kimataifa na Afrika Mashariki.

Mhe Balozi Kombo alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia.

No comments: