Monday, July 22, 2024

WAKALA WA FEDHA AFARIKI KWA KUPIGWA NA KITU KIZITO KICHWANI NJE YA GETI LAKE,MAJAMBAZI WATOWEKA NA MILIONI 47



Mfanyabiashara maarufu mjini Njombe aliyefahamika kwa jina la Godfrey Ndambo (45) ambaye ni mkazi wa uzunguni kata ya Ramadhani amefariki Dunia wakati akipata matibabu mara baada ya kuvamiwa na majambazi waliompiga na kitu kizito kichwani nje ya geti wakati akiingia nyumbani alipokuwa akitoka kazini kwake.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe Mahamoud Banga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema mfanyabiashara huyo alivamiwa Julai 20,2024 majira ya saa mbili na nusu usiku wakati akitoka kwenye shughuli zake za biashara ambapo mpaka sasa Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi juu ya tukio.

"Ndambo alivamiwa wakati anatoka kwenye shughuli zake za biashara wakati anaingia getini na kupigwa na kitu kizito kichwani na waliompiga ambao bado hatujajua idadi yao waliweza kutoweka na fedha ambazo zinakadiriwa kuwa ni Milioni 47 kulingana na taarifa tulizozipata kutoka katika biashara yake ya hesabu zilizofungwa lakini majeruhi alitibwa katika hospitali yetu ya Kibena na baadaye alihamishiwa mkoa wa Mbeya na wakati matibabu yanaendelea akafariki"amesema Kamanda Banga.

Aidha ametoa wito kwa wafanyabiashara ambao wamefunga CCTV camera, muda wote ziwe zinafanya kazi ili kusaidia pia katika uchunguzi kwa kuwa kutokana na tukio hilo waliweza kupata changamoto kwa kuwa camera ndani ya nyumba hiyo ya mfanyabiashara zimfungwa lakini hazifanyi kazi kwa kuwa zilikuwa zimezimwa huku pia akiwaomba wanaofanya shughuli za biashara ya fedha kuweka fedha zao benk buliko kurudi na fedha nyumbani.

No comments: