Wednesday, August 28, 2024

RAIS WA ZANZIBAR NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI MHE.DK.HUSSEIN MWINYI AZUNGUMZA NA MKURUGENZI MKUU WA TAKUKURU IKULU ZANZIBAR


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Crispin Francis Chalamila (kulia kwa Rais) alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikilza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Crispin Francis Chalamila, akiwa na ujumbe wake, alipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo na kujitambulisha leo 27-8-2024, mazungumzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akikabidhiwa zawadi maalum na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Crispin Francis Chalamila, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 27-8-2024, alipofika kwa ajili ya kujitambulisha.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Crispin Francis Chalamila, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar, alipofika kwa mazungumzo na kujitambulisha leo 27-8-2024, na (kulia kwake) Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar Ali Abdalla Ali.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi amezisihi Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) kuongeza ushirikiano kwenye ufanisi wa kazi zao.

Dk. Mwinyi ametoa nasaha hizo, Ikulu, Zanzibar alipozungumza na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Francis Chalamila aliefika kujitambulisha kufuatia uteuzi wa kutumikia nafasi aliyonayo uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.

Rais Dk. Mwinyi amezishauri taasisi hizo mbili kuzidisha ushirikiano hasa kwenye miradi ya kimkakati ya Mendeleo kwa maslahi ya taifa.

Aidha, Dk. Mwinyi amempongeza Mkurugenzi Chalamila kwa uteuzi alioupata na kumtakia heri kwenye majukumu yake mapya.

Pia Rais Dk. Mwinyi amesifu jitihada za ZAECA kwa kuendeleza ufanisi wa makujukumu yao hasa kwenye miradi ya Serikali kwa wanawajibika ipasavyo.

Akizungumza kwa wakati huo bw. Chalamila alimuahidi Rais Dk. Mwinyi kuendeleza ushirikiano uliopo baina ya ZAECA na TAKUKURU katika kufanikisha majukumu yanayowalazimu.

Amesema, TAKUKURU na ZAECA wanashirikiana kwenye mambo mengi tokea waliposaini mkataba wa ushirikiano wao mwaka 2012, ikiwemo kujengeana uwezo, kusihirikana kwenye masuala ya uchunguzi wa kazi zao, kushiriki mikutano ya pamoja ya kikanda na kitaifa.

Vile vile bw. Chalamila alisifu na kupongeza juhudi za maendeleo makubwa zilizofikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Mwinyi.

Alisema, mbali na majukumu mengine walivyonayo TAKUKURU na ZAECA imekua rahisi kwao kushirikiana hasa kuwadhibiti wahalifu wa pande mbili za Muungano wanaojaribu kukimbilia kwenye mipaka ya sehemu hizo Bara na Visiwani.

Bw. Chalamila pia alimuahidi Rais Dk. Mwinyi na Rais Dk. Samia kuendeleza maono yao, na ushauri wao katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi kwa kushirikiana na ZAECA.

Sambamba na kuendeleza mikakati na uchunguzi kwenye miradi ya maendelo na kumuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kwamba wataendelea kusimamia miradi hiyo na kuhakikisha inakamilika kwa viwango vinavyostahiki na kuhakikisha thamani ya fedha za miradi hiyo inaonekana.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan alimteua bw. Chalamila kushika wadhifa alionao sasa Ogasti 14 mwaka huu na kumuapisha Ogasti 15 mwaka huu.

IDARA YA MAWASILINO, IKULU ZANZIBAR.

No comments: