Tuesday, September 3, 2024

KILOSA WAVUKA LENGO USAJILI WAKULIMA RUZUKU YA MBOLEA


Baadhi ya wakulima wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro wakipatiwa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea na kusajiliwa kwenye mfumo wa mbolea ya ruzuku

Na mwandishi Wetu, Kilosa Morogoro
WILAYA ya Kilosa mkoani Morogoro inatajwa kuwa kinara wa matumizi ya mbolea ya ruzuku kati ikilinganishwa na wilaya nyingine za mkoa huo.

Akizungumza wakati wa mkutano na wakulima wa mkoa wa Morogoro uliofanyika wilayani Kilosa, Mkuu wa Wilaya hiyo Shaka Hamdu Shaka alisema licha ya wilaya hiyo kuwa kinara bado ipo haja kwa wataalamu wa kilimo kuwahamasisha wakulima kutumia mbolea kwa usahihi ili kuleta matokeo mazuri zaidi.

Aidha mkuu huyo wa Wilaya aliwakumbusha wakulima kusajiliwa kwenye mfumo wa kidigitali wa mbolea ya ruzuku ili waendelee kunufaika na fursa hiyo inayotolewa na serikali kwaajili ya wakulima wote nchini.

Pamoja na hayo Shaka aliwasisitiza wakulima kuzingatia maelekezo ya wataalam kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya mbolea badala ya kusikiliza kauli za wakulima zinazoposha maana halisi ya mbolea kwenye mmea.

“Serikali imewekeza nguvu kubwa ya hali na Mali kwenye sekta ya kilimo ikiwemo kuajiri maafisa ugani wa kutosha, kuweka ruzuku kwenye mbolea, vitendea kazi kwa maafisa ugani, kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo, jukumu letu wakulima ni kuhakikisha tunazitumia fursa hizo vizuri kwaajili ya matokeo mazuri shambani”, alisema Shaka.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Elizabeth Bolle alisema takwimu za matumizi ya mbolea zinaonesha kuwa Wilaya ya Kilosa kwa msimu wa 2023/24, imetumia jumla ya tani 4,554.8 ikilinganishwa na tani 2,652.1 zilizotumika na wakulima wa wilaya hiyo katika msimu wa 2022/23 sawa na ongezeko la tani 1,902.7

Bolle alibainisha kuwa jumla ya wakulima 23,852 wamesajiliwa kwenye mfumo wa kidijitali ikiwa ni zaidi ya lengo la kusajili wakulima 20,000 wa Wilaya ya Kilosa.

“Pamoja na takwimu hizo Mamlaka inaamini kuwa bado kuna wakulima ambao hawajajisajili, hivyo naomba nitumie nafasi hii kuwasihi wakulima wa Wilaya ya Kilosa na Mkoa wa Morogoro ambao hawajasajiliwa waende kujisajili katika mfumo wa kidijitali kupitia Ofisi za Watendaji wa Vijiji/Mitaa”, alisema Bolle.

Kwa mujibu wa Bolle, pamoja na wakulima kunufaika na mpango wa mbolea ya ruzuku, kanzi data ya usajili wa wakulima itaisaidia Serikali kuweka mipango sahihi ya kuendeleza Sekta ya Kilimo na kuwawezesha wakulima kupata huduma nyingine kama vile huduma za ugani, taarifa za masoko ya mazao, huduma za kifedha na huduma nyinginezo.

Mkoa wa Morogoro unajulikana kwa kilimo cha mazao mbalimbali ikiwemo mahindi, mpunga, miwa, viungo, mbogamboga na matunda, hivyo mkutano huo unaolenga kutoa hamasa ya matumizi sahihi ya mbolea na kuhamasisha usajili kupitia kampeni ya Kilimo ni Mbolea, unatarajiwa kuzaa matunda kwa wakulima kuongeza tija ya uzalishaji.

No comments: