Friday, September 20, 2024

WAZIRI AWESO; SITAKUWA KIKWAZO KWA WANANCHI KUPATA HUDUMA YA MAJI SAFI

Waziri wa Maji Jumaa Aweso, amewahakikishia wananchi wa wilaya ya Mbinga na Nyasa, kupata huduma ya maji safi na salama kutokana na miradi ya maji inayotarajiwa kukamilika hivi karibuni chini ya Wakala wa maji safi na mazingira Vijijini RUWASA katika wilaya hizo.

Ameyasema hayo leo katika ziara yake wilayani Nyasa na Mbinga Mara baada ya kutembelea miradi ya Tingi-Malungu, Miyangayanga pamoja na Matiri, amesema katika kipindi chote ambacho ataiongoza Wizara ya maji hatakuwa kikwazo kwa wananchi hao kupata huduma bora ya maji safi na salama.

Amesema maendeleo ni mchakato na ili kufikia adhima hiyo ni lazima kuwepo na ushirikianao baina ya watendaji wa wizara ya maji pamoja na taasisi zingine hivyo kama wizara wanajukumu lakuhakikisha wanaendelea kushirikiana vyema pamoja kwani wizara hiyo sio ya ukame ambapo watahakikisha maji yanapatikana ya uhakika.

Waziri Aweso ameeleza kuwa kwa asilimia kubwa wanaoteseka na changamoto ya maji ni kinamama hivyo amewaagiza watumishi wa wizara ya maji kuhakikisha watu wenye shida ya maji wanapatiwa huduma hiyo.
Amebaisha kuwa kiasi ya milioni 170 kimetolewa kwaajili ya kusambaza mabomba ya maji Miyangayanga Wilayani Mbinga, na milioni 100 kusambaza mabomba ya maji kijiji cha Tingi, pamoja na kiasi cha milioni 145 kutolewa kwaajili ya kumlipa mkandarasi wa mradi wa Songambele

Akizungumza Mbunge wa Nyasa Eng. Stella Manyanya, amesema kulikuwa na changamoto kwa kinamama wakati wa kujifungua ambao walilazimika kwenda mtoni kuchota maji, huku wengine wakiingia katika migogoro ya kugombania maji katika maeneo ambayo yalikuwa na maji, jambo ambalo lilimlazimu kutumia gharama zake binafsi kutafuta ahueni kwa kuchimba visima hivyo kupitia mradi huo mkubwa utakwenda kuondoa adha ya upatikanaji wa maji katika vijiji hivyo.
Kwa upande wa Mbunge wa Mbinga Mjini Jonas Mbunda ametoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassani pamoja na wizara ya Maji kupeleka mradi wa maji kwenye jimbo lake huku matumaini yake nikwenda kuondoa changamoto zilizokuwepo kwa wananchi wake kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Imeelezwa kuwa mradi wa Tingi-Malungu unatekelezwa na mkandarasi Peace Construction Limited ambao umegharimu kiasi cha Bilioni 1.2 na unatarajia kuhudumia wanakijiji zaidi ya elfu 9600, na unaotarajiwa kukamilika tarehe 30 oktoba mwaka huu, huku mradi wa maji Matiri umegharimu kiasi cha Bilioni 1.6 ambao umefikia asilimia 98 ya utekelezaji.

No comments: