Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imekamilisha ujenzi wa daraja la Msadya lenye urefu wa mita 60 na upana mita 10.5 pamoja na ujenzi wa barabara unganishi ya Kibaoni-Chamalendi-Mdede kwa gharama ya shilingi bilioni 4.2 katika Halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi.
Meneja wa TARURA Wilaya ya Mlele, Mhandisi Paul Mabaya, ameishukuru serikali kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Msadya lenye uwezo wa kupitisha magari tani 30 ambalo limenufaisha wananchi wa kata za Mwamapuli, Chamalendi, Ikuba, Kibaoni na Majimoto kusafirisha mazao yao.
“Daraja hili limekuwa mkombozi, shughuli kubwa hapa ni kilimo na ufugaji, kiasi kikubwa cha mpunga unaolisha nchi yetu unatoka maeneo haya ya Mwamapuli, Lunguya na Chamalendi kuna mashamba makubwa ya mpunga na mahindi hivyo daraja hili limerahisisha usafirishaji wa mazao na mifugo”, alisema.
Aliongeza kuwa Wilaya ya Mlele ina Halmashauri ya Mlele na Halmashauri ya Mpimbwe, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya TARURA katika wilaya hiyo kutoka Bilioni 1 hadi Bilioni 4 kwa mwaka na kwamba wanaendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali ili kuwezesha wananchi kuzifikia huduma za kijamii.
Naye, Mhe. Edward Madiliguntwe, Diwani wa Kata ya Mwamapuli, ameishukuru serikali kwa kutengeneza daraja hilo linalounganisha kata za Mwamapuli na Chamalendi ambalo limesaidia wananchi kusafirisha mazao yao na kukuza shughuli za kibiashara na uchumi.
“Kata hizi zinategemewa sana kwa kuzalisha chakula na kukuza mapato ya hapa na Halmashauri nzima, tunamshukuru Rais Samia kwa kutuletea fedha za daraja hili ambalo limekuwa mkombozi kwetu, zamani wananchi walipata shida kuvuka mto huu ambapo walikuwa wanavuka kwa kubebana lakini sasa wanavuka bila shida yoyote”, alisema.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Chamalendi, Mhe. Yohana Maghembe alisema, kabla ya daraja hilo wananchi kutoka Chamalendi ambao mahitaji yao yapo Majimoto kipindi cha mvua walikuwa wanapata shida kuvuka na kupeleka mifugo yao mnadani eneo la Majimoto, baada ya daraja kujengwa wananchi wanasafirisha mifugo, mazao na bidhaa zao kupeleka viwandani na mnadani bila shida ambapo amemshukuru Mhe. Rais na ameomba TARURA iendelee kuongezewa fedha ili barabara ziendelee kuboreshwa zaidi.
Naye, Bi. Jacquline Philipo mkazi wa kijiji cha Mwamapuli alisema, wajawazito walikuwa wanapata shida kuvuka walikuwa wanajifungulia njiani lakini sasa wanaishukuru serikali kwa kuwajengea daraja ambapo kwa sasa wanafika hospitali kwa wakati.
Bw. Sylvester Kibigi mkazi wa Majimoto amesema, kabla ya daraja kujengwa kipindi cha mvua pikipiki zilikuwa zinasombwa na maji, kwasasa wanapita bila shida baada ya daraja na ameiomba serikali kuendelea kuwaboreshea barabara kutoka darajani kwenda Mabambasi hadi Useja, barabara ya Chamalendi-Sentakichaa na barabara kutoka darajani hadi Majimoto ili ziweze kupitika katika nyakati zote.
No comments:
Post a Comment