Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya ICGLR Balozi Jao Samuel Caholo akizungumza kwenye ufunguzi kikao cha Waratibu wa Kitaifa ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Waziri wa Mambo ya Nje (RIMC) wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) unaotarajiwa kufanyika tarehe 24 Novemba 2024 jijini Luanda, Angola.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika, katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi. Ellen Maduhu akifuatilia kikao cha Waratibu wa Kitaifa kilichokuwa kikiendea jijini Luanda Angola tarehe 21 Novemba 2024.
Meza Kuu wakiongoza Kikao cha Waratibu wa Kitaifa cha ICGLR kikiendelea jijini Luanda, Angola.
Watendaji na Viongozi wa sekta mbalimbali kutoka Nchi wanachama wa Jumuiya ya Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) wanatarajiwa kukutana jijini Luanda, Angola kujadili kuhusu hali ya amani na usalama katika ukanda huo kwenye mkutano utakaofanyika tarehe 24 Novemba 2024.
Mkutano huo utakao husisha Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi Wanachama wa ICGLR unalenga kujadili na kutatua changamoto za amani na usalama katika eneo la ukanda huo hususan nchi za Jamhuri ya Sudani, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mbali na hayo mkutano huo utajadili suala la kumpata Mwenyekiti ajaye atakayeongoza Jumuiya hiyo kwa kipindi cha miaka miwili ijayo baada ya wa sasa Angola kumaliza muda wake, na kupendekeza Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya kufuatia ya wasasa kumaliza kipindi chake cha kuhudumu.
Maandalizi ya mkutano huo yalianza tarehe 11 Novemba 2024 kwa vikao mbalimbali katika ngazi ya wataalamu ikiwemo wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, Wataalamu wa masuala ya jinsia, wataalamu wa masuala ya fedha, Mawaziri wa Ulinzi na Waratibu wa Kitaifa kutoka nchi wanachama waliokutana leo tarehe 21 Novemba 2024.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha Waratibu wa Kitaifa, Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya ICGLR Balozi Jao Samuel Caholo ameeleza kuwa licha ya jitihada jinazoendelea na mafanikio yaliyopatikana katika kurejesha na kudumisha hali ya amani na usalama kwenye ukanda wa maziwa Makuu, bado juhudi zaidi zinahitajika kutoka nchi wanachama ili kupata suluhu ya kudumu dhidi ya migogoro hiyo.
Balozi Caholo ameongeza kusema kuwa suala la kulinda amani na usalama katika ukanda wa maziwa makuu ni muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya wananchi wa ukanda huo.
Kadhalika, emetoa wito kwa nchi wanachama kupitia Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Angola kuongeza juhudi katika kushughulia hali ya kuzorota kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi za DRC na Rwanda na Bunduri na Rwanda.
“Amani na usalama katika ukanda wetu unategemea zaidi utayari na juhudi zetu wenyewe katika kutafuta suluhu ya changamoto zinazotukabili, hivyo ni mtarajio ya wengi kuwa mkutano huu muhimu utasaidia kufikia malengo ya kuwa na ukanda wenye amani ya kudumu kwa mustakabali mwema wa kizazi chetu na kijacho” Alieleza Balozi Caholo.
Vilevile, mkutano huo utapokea na kujadili taarifa ya hali ya utendaji wa Sekretarieti ya IGCLR kwa kuangazia ufanisi wa maeneo mbalimbali ikiwemo mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024, hali ya utoaji michango ya nchi wanachama, rasilimali watu na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mpango mkakati wa mwaka 2022 -2026.
Katika hutua nyingine kikao hicho cha Waratibu wa Kitaifa kilichofanyika leo tarehe 21, kimetoa pole kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufatia maafaa yaliyotokana na kuporomoka kwa jengo yaliyotokea hivi karibuni katika eneo la Kariakoo, jijini Dar es Salaa.
Aidha mkutano huo umetoa pongezi kwa Serikali ya Tanzania chini ya Uongozi wa Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuchuka hatua za haraka katika kushugulikia janga hilo ikiwemo kuokoa watu walioangukiwa na jengo na kutoa huduma muhimu ikiwemo matibabu kwa majeruhi.
Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo ngazi ya Waratibu wa Kitafa umeongozwa Bi. Ellen Maduhu, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Afrika, katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
ICGLR yenye makao makuu yake jijini Bujumbura, Burundi ilianzishwa mwaka 2007, na ina jumla ya Nchi Wanachama 12, ambao ni Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Kongo, DRC, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania, Uganda na Zambia.
No comments:
Post a Comment