ANGALIA LIVE NEWS

Friday, November 22, 2024

SERIKALI KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA


Mwenyekiti wa Kongamano la Kodi, Bw. Robert Manyama, akitoa ufafanuzi kwa wafanyabiashara na wadau mbalimbali (hawamo pichani) katika Kongamano la Kodi lililofanyika jijini Arusha, kulia kwake ni Afisa Mtendaji wa TCCIA Mkoa wa Arusha Bi. Sia Maruda.
Baadhi ya washiriki waliohudhuria Kongamano la Kodi wakisikiliza maoni yaliyotolewa na wafanyabiashara mbalimbali waliohudhuria katika Kongamano la Kodi lililofanyika jijini Arusha.
Na. Eva Ngowi, WF - Arusha

Serikali imeahidi kuendelea kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji ili kuchochea ukuaji wa sekta mbalimbali kama Utalii, Kilimo, Madini, Viwanda, Uvuvi na Ufugaji, kulinda viwanda vya ndani, kuvutia mitaji na uwekezaji nchini, kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani, kuchochea ulipaji kodi kwa hiari na kuboresha usimamizi na ukusanyaji wa kodi, ada na tozo mbalimbali.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kongamano la Kodi, Bw. Robert Manyama, wakati wa zoezi linaloendelea la kupokea na kukusanya maoni kwa wataalam na washauri wa kodi, wadau wa sekta mbalimbali nchini, wafanyabiashara, wazalishaji wa bidhaa na mazao mbalimbali kwenye Kongamano la Kodi lililofanyika jijini Arusha.

Bw. Manyama alisema mojawapo ya maoni yaliyotolewa mwaka jana yalifanyiwa kazi ikiwemo kusamehe VAT kwenye Vifaa na Mitambo ya kuchakata na kuhifadhi mazao ya nyuki, kusamehe VAT kwenye kwenye chai inayotengenezwa ndani ya nchi (Local Blended Tea) pamoja na Kutoza VAT kwa kiwango cha asilimia 0 kwenye madini ya dhahabu yatakayouzwa kwa Viwanda vya Kusafisha Madini ya Dhahabu nchini.

Alisema, Serikali pia imetoa unafuu wa kutolipa kodi ya mapato mbadala (Altenative Minimum Tax) kwenye kampuni zinazochakata mazao ya chai, kupunguza ushuru wa bidhaa kutoka shilingi 63.80 hadi shilingi 56 kwa lita ya maji ya kunywa yaliyosindikwa, kuanzisha vyanzo kwa ajili ya kugharamia Bima ya Afya kwa watu wasio na uwezo na makundi maalum hususan wanawake, wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano pamoja na kuongeza ushuru wa forodha kwenye baadhi ya bidhaa zinazoingizwa nchini ili kulinda viwanda vya ndani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Mkoa wa Arusha ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Usafirishaji Mkoa wa Arusha, Kilimanjaro na Manyara, Bw. Locken Massawe, alitoa shukurani zake kwa Serikali kwa kuonesha umuhimu wa kuwakutanisha na kusikiliza maoni yao.

“Kwa sasa hivi tunaona tofauti kabisa na kule tulikotoka kwa sababu hata ukiangalia kwa sasa hivi muundo uliotumika wa kuchukua maoni ni ile staili inayokufanya wewe mwenyewe unapata imani kwamba linalokwenda mbele ya Serikali litafanyiwa kazi na serikali imelipa kipaumbele” alisistiza Bw. Massawe.

Naye Mtunza Hazina wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Mkoa wa Arusha, Bi. Ester Msule, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kupitia Wizara ya Fedha na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) kwa kuwaletea Kongamano hilo lililowawezesha kutoa maoni yao wakiwa na imani kubwa kwamba, yatafanyiwa kazi kama walivyoyawasilisha na kuwaletea mabadiliko katika biashara zao na kulipa kodi stahiki kwa manufaa ya Taifa la Tanzania.

“Naishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na TCCIA kuleta Kongamano kama hili na tunapata fursa ya kuja kujieleza sisi kama wakulima na wafanyabiashara kwa ujumla kwa sababu sisi viongozi nyuma yetu kuna wafanyabiashara wengi na nyuma yetu tumebeba wafanyabiashara wakubwa kwa hiyo tumemshukuru sana Mhe. Rais pia kutuletea Kongamano kama hili na tumekuja tumejifunza mambo mengi sana; kwanza Mama ametuheshimisha kutusikiliza sisi Jumuiya ya Wafanyabiashara ili tuwawakilishe wenzetu wengine. Kwa hiyo tunashukuru Wizara ya Fedha imesikiliza kero zetu na tunajua watakwenda kuyafanyia kazi haya tuliyoyaeleza.” Alisema Bi. Msule.

Aidha, Afisa Mtendaji wa TCCIA Mkoa wa Arusha, Bi. Sia Maruda, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutaka kuboresha mfumo wa kodi Tanzania lakini pia ameishukuru Wizara ya Fedha kwa kutembelea Mkoa wa Arusha ili kujua kero na changamoto za kodi zinazowakabili wafanyabiashara.

“Kupitia kongamano hili tunaamini “Finance Bill” inayokuja maboresho yaliyotolewa yatawasilishwa vizuri na wafanyabiashara wameweza kupata suluhisho. Tunachotaka sisi ni kujenga nchi yetu kwa pamoja, hatutaki kukweka kodi na wala hatushauri kukwepa kodi lakini tunataka kujenga mazingira ambayo mfanyabiashara atafanya biashara bila kuona kwamba anakandamizwa.” Alisisitiza Bi. Marunda.

No comments: