*Asema Rais Dkt. Samia anathamini mchango wa China kwenye maendeleo nchini
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika hafla ya Kumbukumbu ya Miaka Kumi ya Jumuiya ya kukuza Ushirikiano kati ya China na Tanzania iliyofanyika kwenye ukumbi wa Maktaba Mpya ya Chuo Kiki cha Dar es salaam
Na.Hassan Silayo
WAZIRI MKUU Mhe.Kassim Majaliwa amesema kuwa uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na China umeendelea kukua ambapo mwaka 2023 biashara kati ya nchi hizo ilifikia dola bilioni 8.78.
Amesema kuwa ukuaji na ushirikiano huo wa makampuni ya China na wafanyabiashara wa Tanzania umeleta maendeleo katika ukuaji wa viwanda vya ndani, kutengeneza ajira, ujenzi wa miundombinu na uboreshaji wa hali ya maisha ya Watanzania.
Amesema hayo (Novemba 30, 2024) wakati wa hafla ya Kumbukumbu ya Miaka Kumi ya Jumuiya ya Kukuza Ushirikiano kati ya China na Tanzania, iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo Kikuu cha Dar ea Salaam, Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa Kampuni za China zimezindua takribani miradi 1,274 ambayo kwa kiasi kikubwa pamoja na mambo mengine, imezalisha ajira kwa Watanzania. “Huu ni uthibitisho wa jinsi ushirikiano wetu unavyolenga kutoa fursa kwa wananchi wetu”.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan anathamini mchango wa China katika maendeleo ya Tanzania kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za biashara, miundombinu na utamaduni”
Aidha amesema kuwa China ni moja ya mshirika mkubwa wa kibiashara na uwekezaji kwa Tanzania na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo kwenye sekta za kilimo, madini, viwanda na maendeleo ya miundombinu.
Ameongeza kuwa China imekuwa mshirika muhimu katika kuisaidia Tanzania kukabiliana na majanga ya kiafya ikiwemo magonjwa ya kuambukiza na changamoto za afya ya mama na mtoto. “China imekuwa ikitoa timu za wataalam, kuchangia vifaa, na kusaidia kujenga miundombinu ya afya. Ushirikiano huu umeokoa maisha ya wengi na umehakikisha kwamba watu wetu wanapata huduma bora za matibabu”
akizungumza kuhusu Jumuiya ya Kukuza Urafiki kati ya Tanzania na China, Mheshimiwa Majaliwa amesema jumuiya hiyo imekuwa mchango mkubwa katika kukuza na kuendeleza uhusiano kati ya mataifa hayo mawili imiwemo kimeleta watu pamoja, si tu kutoka kwa serikali, bali kutoka nyanja mbalimbali za maisha.
Akizungumza kwa Niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Naibu Waziri wa Wizara hiyo Cosato Chumi amesema kuwa jumuiya hiyo imeendelea kutumika kama msingi wa kukuza maelewano na ushirikiano kupitia sekta za elimu, afya, utamaduni na biashara
Naye, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo na Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda amesema jumuiya hiyo ni matunda ya mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na China ambayo kwa kipindi kirefu yamechangia kwa kiasi kikubwa kukuza na kuwezesha maendeleo nchini kwenye sekta mbalimbali ikiwemo Miundombinu, kilimo, Biashara na Afya.
(mwisho)
No comments:
Post a Comment