ANGALIA LIVE NEWS

Monday, December 2, 2024

MAKAMU WA RAIS AKIIFARIJI FAMILIA YA DKT MASHINDANO


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisaini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha aliyewahi kuwa Msajili wa Hazina marehemu Dkt. Oswald Mashindano wakati alipowasili nyumbani kwa marehemu Kijichi Jijini Dar es Salaam tarehe 29 Novemba 2024.


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango na Mkewe Mama Mbonimpaye wakiifariji familia ya marehemu Dkt. Oswald Mashindano ambaye aliwahi kuwa Msajili wa Hazina wakati walipofika nyumbani kwa marehemu Kijichi Jijini Dar es Salaam

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameifariji familia ya aliyewahi kuwa Msajili wa Hazina Marehemu Dkt. Oswald Mashindano aliyefariki tarehe 27 Novemba 2024.

Makamu wa Rais ameambatana na Mwenza wake Mama Mbonimpaye Mpango na kusaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa marehemu Kijichi Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waombolezaji, Makamu wa Rais amesema marehemu Dkt. Oswald Mashindano amefanya kazi vizuri na kwa uaminifu mkubwa enzi za uhai wake. Amesema katika nafasi mbalimbali alizowahi kutumikia ikiwemo Msajili wa Hazina aliweza kutoa mchango mkubwa katika Taifa.

Aidha amesema marehemu Dkt. Mashindano ametoa mchango wa maendeleo ya Taifa kupitia tafiti mbalimbali alizowahi kufanya hususani tafiti za maendeleo ya kilimo.

Marehemu Dkt. Oswald Mashindano atazikwa katika makaburi ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam tarehe 30 Novemba 2024.

No comments: