
Mwanamke anayesadikika mchawi aliyekutwa katika ofisi za TANESCO Ruvuma akisitiriwa kwa kuvishwa kitenge
Na Regina Ndumbaro - Ruvuma .
Taharuki imetanda katika Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, baada ya mwanamke mmoja kupatikana akiwa uchi ndani ya uzio wa ofisi za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia Machi 11, 2025, na limesababisha mijadala mikubwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo.
Kwa mujibu wa mashuhuda, mwanamke huyo anadaiwa kuwa alikuwa akisafiri kwa njia za kishirikina kwa kutumia ungo kutoka wilaya ya Masasi, mkoani Mtwara, kuelekea wilaya ya Nyasa.
Hata hivyo, safari yake ilikatizwa ghafla baada ya kupoteza mwelekeo na kuanguka ndani ya uzio wa ofisi hizo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa mwanamke huyo ana matatizo ya akili.
Ameongeza kuwa uchunguzi wa kina unafanyika ili kubaini chanzo halisi cha tukio hilo na hali ya mwanamke huyo.
Wananchi wa Songea wameshtushwa na tukio hilo, huku baadhi wakidai ni ushahidi wa uwepo wa vitendo vya kishirikina, ingawa serikali haitambui imani kama hizo.
Mwanamke huyo kwa sasa amelazwa hospitalini kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu na mahojiano zaidi.
No comments:
Post a Comment