Na John Walter -Kiteto
Watumishi watatu wa serikali za vijiji katika Kijiji cha Engusero, wilayani Kiteto, wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashtaka nane, yakiwemo matumizi mabaya ya madaraka na uhujumu uchumi.
Watuhumiwa hao ni Robati Mchambui, Mwenyekiti wa Kijiji cha Engusero, Mwachiwa Mgome, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Engusero, na Jorome Maiko, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mabululu. Kwa mujibu wa Mwendesha Mashtaka Yahaya Masaa Kilija, watuhumiwa hao wanakabiliwa na makosa yaliyo kinyume na Kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.
Watuhumiwa wanadaiwa kuuza ekari 10.5 za ardhi ya kijiji kinyume na Kifungu cha 8(5) cha Sheria ya Ardhi ya Kijiji, Sura ya 114, kama ilivyorekebishwa mwaka 2019. Mwendesha mashtaka aliieleza Mahakama ya Wilaya ya Kiteto, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Boniface Lihamwike, kuwa watuhumiwa hao walihusika katika makosa hayo kwa nyakati tofauti, wakitumia nafasi zao kwa makusudi.
Katika shtaka la nane, watuhumiwa wanadaiwa kujipatia kiasi cha shilingi milioni 2.6 kutokana na mauzo ya ardhi hiyo, jambo ambalo ni ubadhilifu wa fedha za umma.
Mahakama imeeleza kuwa dhamana ya watuhumiwa iko wazi, lakini walishindwa kutimiza masharti ambayo yanahitaji kila mtuhumiwa kuwa na wadhamini wawili wanaotakiwa kuwa watumishi wa serikali na kuwa na dhamana ya shilingi milioni tano kwa kila mmoja. Hadi sasa, washtakiwa wanaendelea kubaki mahabusu wakisubiri kutimiza masharti ya dhamana.
No comments:
Post a Comment