ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 2, 2026

KHANGA NI KITABU KINACHOTEMBEA, TABIA NJEMA VAZI LA KUDUMU - FARIDA SEKIMONYO

 



Dar es Salaam - Mgeni Rasmi wa Tamasha la Kanga 2026, Bi Farida Sekimonyo Mkurugenzi wa kampuni ya Faith and Entertainment  amesema khanga si kitambaa tu bali ni historia, maarifa na utambulisho wa jamii. Akizungumza Nov 1, 2026 Kijiji cha Makumbusho kwenye tamasha la Khanga 2026 lililoandaliwa na Dira Women Organization (DIWO) chini ya Bi Shamsa Juma Danga,

Amesema kanga ni kitabu kinachotembea. "Maneno ya kwenye khanga hayapaswi kuwa mapambo tu. Khanga ni vazi linalochakaa lakini tabia njema ni vazi la kudumu. Khanga inayosema Subira huvuta heri itukumbushe kuwa na subira."

Kwenye tamasha hilo ameagiza watoto 25 walioshiriki kuonesha mavazi hayo ya ubunifu wa mitindo kufunguliwa akaunti Azania Bank ambapo atagharamia fedha za awali, kama kumbukumbu ya kudumu na kuwajengea utamaduni wa akiba.

Amesema khanga inachangia uchumi na utalii kupitia magauni, mikoba na zawadi za utalii. Ameshauri ubunifu wa khanga zenye mandhari ya Kilimanjaro na wanyamapori. Amesema AFCON 2027 ni fursa ya kutangaza kanga kimataifa.

"Vazi la Taifa na utambuzi wa UNESCO vinahitaji mjadala na utafiti. Kidole kimoja hakivunji chawa na khanga isiishie kuwa kumbukumbu ya jana iwe fahari ya leo na fursa ya kesho," amesema Bi. Farida Sekimonyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa DIWO Bi Shamsa Danga amesema lengo ni kuwarithisha watoto utamaduni hususani kanga. "Wazazi wetu wameturithisha kanga, kizazi cha 2000 hawajui. Mtoto anapozaliwa anavikwa kanga na kwa Waislamu mpaka kaburini jeneza linawekwa na kanga."

Nae Mwanzilishi wa Usiku wa Kanga za Kale, Bi Asya Idarous Khamsin anayeishi Marekani amesema jukwaa hilo lilibeba wabunifu chipukizi na sasa ni wakubwa ndani na nje. "Awali ilikuwa kwa taabu lakini lilikua na kuwa kubwa nchini."

"Kanga ina historia, ukizaliwa unapewa kanga, ukioga unapewa kanga kujifuta, kazi yake ni kubwa na ina thamani na inanunuliwa sana nje na ndani," amesema Asya.

Tamasha limehudhuriwa na Serikali, BASATA, taasisi za utamaduni na wadhamini Azania Bank na wengine wengi.

















No comments: