SERIKALI kupitia kongamano la Tanzania Fashion Forum 2026 imesema sekta ya ubunifu wa mavazi ina mchango mkubwa katika uchumi wa nchi, ikiwemo kuzalisha ajira, kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na kuitangaza Tanzania duniani.
Akifungua kongamano hilo November 24, 2026 Jijini Dar es salaam kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara Sempeo Manongi amesema mitindo na mavazi sio urembo tu, ni tasnia inayounganisha kilimo, viwanda, biashara, utamaduni, utalii na huduma.
Amesema sekta ya nguo na ubunifu ina mchango mkubwa katika uchumi, inazalisha ajira hasa kwa vijana na wanawake, inapunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje na inaitangaza Tanzania duniani.
Manongi amesema Wizara inataka kuona wabunifu wa leo wakigeuka kuwa wamiliki wa viwanda vikubwa vya nguo na mavazi kesho, kwa kuimarisha mnyororo wa thamani wa pamba, nguo na mavazi na kuwawezesha wajasiriamali kupata mitaji, ujuzi na teknolojia.
Aidha, amewataka wabunifu hao kuimarisha ubora, urasimishaji na haki miliki kupitia BRELA na TBS, kukuza chapa ya Made in Tanzania, kupanua masoko kupitia teknolojia na fursa za jumuiya za Afrika kama EAC, SADC na AfCFTA, na kuhamasisha uwekezaji na uzalishaji endelevu.
Kwa wabunifu na wajasiriamali, Manongi amewataka wasidharau mwanzo mdogo, waendelee kujifunza, kuboresha bidhaa zao, kushirikiana na kuthubutu kuingia katika masoko mapya, kwani Tanzania inaweza kuwa kitovu cha uzalishaji wa nguo na ubunifu wa mavazi barani Afrika.
"Azma ya Serikali ni kuona pamba yetu ikichakatwa nchini, vitambaa vikizalishwa nchini, mavazi yakibuniwa na kutengenezwa nchini, chapa zikimilikiwa na Watanzania na bidhaa zetu zikiuzwa duniani.
Tuthamini bidhaa zetu, tuvae bidhaa zetu, tujenge viwanda vyetu." amesema Manongi.
Kwa upande wake, Mustafa Hassanali ameishukuru Serikali kwa kuwezesha baadhi ya wabunifu kupata mikopo. Hata hivyo, ametumia fursa hiyo kuiomba Serikali kupitia bajeti ya 2028/29 kuona namna ya kuwasaidia zaidi wabunifu, hususan vijana, ili waweze kukua na kushindana katika soko la ndani na la kimataifa.
Katika kongamano hilo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo suala la changamoto za uzalishaji wa bidhaa za nguo, masoko na namna ya Wabunifu kupata mitaji na fursa za kibiasha kupitia ubunifu wa mavazi.
Kongamano hilo limeandaliwa na 361 Degrees Afrika kwa kushirikiana na wadau wengine wakiwemo CRDB Bank Plc, kampuni ya bia ya Serengeti, Mustafa Hassanali Foundation na Fashion Association of Tanzania.




























No comments:
Post a Comment