Kikosi Kazi cha Kitaifa cha Kuharakisha Uwekezaji katika Viwanda vya Bidhaa Tiba (PIAT) kimeridhishwa na hatua iliyofikiwa katika uanzishaji wa viwanda vya bidhaa tiba katika Kongani ya Viwanda ya Mloganzila, kufuatia ziara ya kikosi hicho iliyofanyika tarehe 8 Novemba 2026.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyoongozwa na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb), ilielezwa kuwa matunda ya uwekezaji huo yanatarajiwa kuanza kuonekana kuanzia Mei 2027, ambapo uzalishaji wa takribani asilimia 60 ya vifaa tiba unatarajiwa kuanza.
Waziri wa Afya alisisitiza uwepo wa soko la uhakika kwa wawekezaji wa bidhaa tiba, siyo tu nchini Tanzania, bali pia katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, akiwahimiza kutumia fursa zilizopo kuwekeza nchini.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Viwanda vya Dawa, Mhe. Emmanuel Tayari, alieleza kuwa eneo lote la kongani hiyo tayari limepata wawekezaji, ambao wamewasilisha mipango kazi yao. Aliongeza kuwa Kampuni ya Hongyu, yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha na kuuza vifaa tiba katika soko la Ulaya, inaendelea kukamilisha ujenzi wa majengo yatakayotumika kwa ajili ya kuanzisha viwanda vya vifaa tiba nchini.
Kongani ya Viwanda ya Mloganzila, iliyopo Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam, ilizinduliwa tarehe 8 Mei 2026 na ina ukubwa wa takribani ekari 450. Kongani hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kukuza uzalishaji wa ndani wa bidhaa tiba, kupunguza utegemezi wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na kuimarisha upatikanaji wa bidhaa tiba nchini.
PIAT inaundwa na wataalamu kutoka sekta za afya, viwanda na uwekezaji, chini ya usimamizi mkuu wa Wizara ya Afya, kwa lengo la kuratibu na kuharakisha uwekezaji katika viwanda vya bidhaa tiba nchini.















No comments:
Post a Comment