ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, February 17, 2010

Wajitosa kupitia upya hukumu ya Babu Seya!

aliyekuwa akiwatetea mwanamuziki Nguza Viking 'Babu Seya' na wanawe, Mabere Marando amesema mawakili kadhaa wamejitolea kupitia hukumu ya mwanamuziki huyo ili waiombe mahakama kuipitia upya.

Akizungumza ktk mahojiano na kituo kimoja cha Tv juzi, Marando alisema mawakili hao sasa wanapitia hukumu hiyo kifungu kwa kifungu na kwamba wakigundua makosa, watafungua marejeo hayo ambayo yatafanyiwa kazi na jopo la majaji saba.

Rufaa iliyothibitisha adhabu ya kifungo cha maisha kwa mwanamuziki huyo iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Kisutu, ilisikilizwa na jopo la majaji watatu.

"Sitawataja majina yao, lakini tayari jopo la mawakili limeanza kazi ya kupitia kifungu kwa kifungu hukumu ya mzee Nguza ili kuona kama kuna makosa ya kisheria tuweze kufungua 'review' (marejeo) kabla siku 60 hazijaisha."

"Ila ni kwamba hatutaenda kufungua marejeo kabla ya kujiridhisha kwanza kama kuna makosa ya kisheria na tukibaini kwamba kuna asilimia kubwa ya kushinda, tutafungua marejeo, kwani wapo watu walishawahi kufungua na kushinda," alisema Marando.

Marando alisema mawakili hao, walijitolea kwa mapenzi yao kwa Babu Seya na mwanaye pamoja na kunyoosha sheria ya Tanzania kwa maslahi ya watanzania wote.

"Mawakili hawa wenzangu waliniambia kuwa kuna makosa ya kisheria ktk hukumu lakini, mimi nikawambia nimekuwa na hii kesi kwa muda mrefu na inawezekana baadhi ya mambo nisiyaone, kwa hiyo fanyeni mapitio ya hukumu ili tuone kama tunaweza kufungua marejeo na kushinda.

"Kwa hiyo mawakili hawa wamejitolea si tu kwa mapenzi yao kwa mzee Nguza bali pia kwa mapenzi ya kutaka kunyoosha sheria ili iweze kunyooka,"alisema Marando.

No comments: